1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu kampuni ya Opel kuchukua muda

Charo Josephat/ AFP 6 Machi 2009

Serikali ya Ujerumani yashindwa kufikia makubaliano na viongozi wa kampuni ya General Motors barani Ulaya

https://p.dw.com/p/H6z5
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Karl-Theodor zu Guttenberg (kushoto) na kiongozi wa kampuni ya Opel Carl-Peter Forster (kulia) leo Ijumaa Machi 6 baada ya kukutana mjini BerlinPicha: AP

Mazungumzo kuhusu mpango wa kuinusuru kampuni ya magari ya Opel hapa Ujerumani inayomilikiwa na kampuni ya General Motors ya Marekani yamemalizika leo mjini Berlin bila kupatikana ufumbuzi. Serikali ya Ujerumani imesema itachukua majuma kadhaa kabla kupitisha uamuzi kuhusu uwezekano wa kuisadia kifedha kampuni ya Opel.

Mazungumzo yatachukua wikikadhaa kwa kuwa pande zinazohusika zinatambua kuna maswali mengi yanayohitaji kujibiwa, amesema msemami wa serikali ya Ujerumani, Ulrich Wilhelm, kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin, muda mfupi baada ya kumalizika mkutano kati ya wakurugenzi wa kampuni ya Opel na kampuni mama ya Marekani, General Motors.

Waziri wa uchumi, Karl-Theodor zu Guttenberg, amekutana na kiongozi wa kampuni ya General Motors barani Ulaya, Carl-Peter Forster, kujadiliana kuhusu ombi la kampuni hiyo kutaka yuro bilioni 3.3 kama msaada kutoka kwa serikali. Viongozi wa kampuni hiyo sharti waishawishi serikali ya Ujerumani iunge mkono mpango wa mageuzi ambao kufikia sasa umekuwa ukiungwa mkono. Wametakiwa watoe maelezo zaidi ya maswali kuhusu biashara ya kampuni ya Opel na mipango ya kuifanya kampuni hiyo iweze kupata faida.

Maafisa wa Ujerumani wana wasiwasi kwamba hali ya kampuni ya Opel kuitegemea sana kampuni ya General Motors, itasababisha sehemu ya msaada wa fedha za serikali kuhamishwa nchini Marekani. Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Karl Theodor zu Guttenber anatarajiwa kwenda nchini Marekani mwezi huu kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni ya General Motors na maafisa wa serikali ya Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Ujerumani, kampuni ya General Motors imetoa haki miliki za kampuni ya Opel ya hapa Ujerumani kwa benki kuu ya Marekani ili ipatiwe msaada wa fedha za umma. Wakati huo huo, Ujerumani imeanza kutafuta njia za kuisadia kampuni ya Opel inayowaajiri wafanyakazi 26,000 hapa nchini na 50,000 katika nchi za Ulaya.

Kwenye mkutano wa serikali ya mseto ya Ujerumani, mbunge wa chama cha Social Democtaic, SPD, Peter Struck, amenukuliwa na gazeti la Hannoversche Allgemeine, akisema na hapa namnukulu, Tumekubaliana kwamba tunataka kuisaidia kampuni ya Opel", mwisho wa kumnukuklu kiongozi huyo. Swali kubwa ni mfumo wa msaada huo wa serikali.

Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu, hatima ya kampuni ya Opel imekuwa swala linalozungumziwa sana. Baadhi ya viongozi wa Ujerumani wameelezea kusita kwao kuhusiana na mpango wa kuinusuru kampuni hiyo, wanayoiona kutokuwa na umuhimu katika uchumi wa nchi hii. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble amesema leo kwamba kwampuni ya Opel inatakiwa kutafakari kwa makini ulinzi kwa mujibu wa sheria kuhusu muflisi.