1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran

Oummilkheir21 Agosti 2007

Ali Larijani aonya dhidi ya vikwazo vya jumuia ya kimataifa akisema vitazidi kukorofisha mambo

https://p.dw.com/p/CH9K
Mtambo wa kinuklea wa Iran
Mtambo wa kinuklea wa IranPicha: AP

Mazungumzo kati ya Iran na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki –IAEA yameingia siku yake ya pili na ya mwisho hii leo .Mkuu wa tume ya Iran , Ali Larijani ameonya vikwazo vipya vya baraza la usalama dhidi ya nchi yake vinaweza kuvuruga matokeo ya mazungumzo hayo.

Mazungumzo haya yaliyoanza jana mjini Teheran ni duru ya tatu katika mlolongo wa mazungumzo yaliyolengwa kutathmini “mpango wa kimkakati “uliopendekezwa na Iran.

Ikitiwa kishindo na umoja wa mataifa izuwie mradi wake wa kurutubisha maadini ya Uranium,Iran ilikubali mwezi June uliopita kuandaa kwa kipindi cha siku 60 “mpango wa kimkakati” utakaorahisisha shughuli za wataalam wa shirika la kimataifa la nguvu za nishati , kuvitembelea vinu vyake vya kinuklea na kufafanua kwa undani zaidi kinachofanyika nchini humo.

Ujumbe wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki unaoongozwa na naibu mwenyekiti Olli Heinonen walianza duru hii mpya ya mazungumzo kwa kuzungumza na afisa wa usalama wa taifa wa Iran Javad Vaeedi.

Hakuna habari zilizotangazwa mwishoni mwa mazungumzo ya jana na haijulikani pia kama viongozi hao wawili watazungumza na waandishi habari au la mazungumzo yao yatakapomalizika hii leo.

Mabwana Vaeedi na Heinonen, wameshawahi kukutana duru mbili za mwanzo zilipofanyika mijini Teheran na Vienna-lakini duru hii ya sasa inaangaliwa kua muhimu kupita kiasi na ya mwisho itakayoamua kama Iran iwekewe vikwazo zaidi na jumuia ya kimataifa.

Jumuia ya kimataifa na hasa Marekani inaituhumu Iran kutaka kutengeneza silaha za kinuklea kwa kisingizio cha nishati ya kinuklea.Rais George W. Bush wa Marekani anasema:

“Tunachokitaka ni kuwazuwia wasiwe na nguvu za kurutubisha maadini ya Uranium hadi kua na uwezo wa kutengeneza silaha ya kinuklea.”

Mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo pamoja na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki,Ali Larijani ameonya hii leo,vikwazo vyovyote vya baraza la usalama dhidi ya nchi yake vitafuja ushirikiano wa Iran na taasisi hiyo ya kimataifa na kusababisha mazungumzo yasilete tija yoyote.

Kwa mujibu wa televisheni ya taifa nchini Iran,Ali Larijani ameikosoa Marekani kwa kufifiisha maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa kati ya Iran na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki-kwa lengo tunanukuu:” la kuchochea mashaka ili kufungua njia ya kutangazwa vikwazo.

Matokeo ya mazungumzo yaliyoanza jana mjini Teheran yatakua kiini cha ripoti itakayowasilishwa na mkuu wa shirika la IAEA Mohammed Al Baradei katika mkutano wa shirika hilo mwezi ujao .Ripoti hiyo ndio itakayofafanua kama maendeleo yamepatikana au la.