1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kumaliza uhasama Sudan

24 Septemba 2012

Marais wa Sudan na Sudan Kusini wameanzisha mazungumzo kumaliza uhasama kati ya nchi zao. Katika mazungumzo ambayo yanafanyika nchini Ethiopia, unatafutwa muafaka juu ya masuala nyeti kama vile mafuta na mpaka.

https://p.dw.com/p/16DAN
Wajumbe wa Sudan na Sudan Kusini wanakutana mjini Addis Ababa
Wajumbe wa Sudan na Sudan Kusini wanakutana mjini Addis AbabaPicha: Reuters

Rais Omar al-Bashir wa Sudan na mwenzake wa Sudan Kusini, Salva Kiir, wamekutana usiku wa kuamikia leo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, Mazungumzo yao ya muda wa masaa mawili yameanzisha mchakato wa kutafuta suluhu kwa matatizo katika uhusiano wa nchi hizo jirani, ambazo hadi Julai mwaka jana zilikuwa nchi moja.

Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Atif Kiir, amesema bado zipo tofauti kati ya pande mbili zinazozungumza, ila akaelezea imani kwamba pengo lililopo litapungua hadi kufikia makubaliano.

Marais waongoza njia

Rais Al-Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan Kusini
Rais Al-Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan Kusini

Marais al-Bashir na Salva Kiir walizungumza hadi usiku wa manane, na ripoti za waandishi zinasema walitoka ndani ya chumba cha mkutano wakionekana wachangamfu. Mazungumzo yao yanaendelea leo hii, pengine chini ya upatanishi wa waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.

Badr el-din Abdullah, msemaji wa serikali ya Khartoum pia anakubaliana na mwenzake wa Sudan Kusini kwamba bado yapo mambo ambayo hayajaafikiwa, na kuongeza kuwa masuala ya kiusalama ndiyo changamoto kubwa iliyopo.

Balozi wa Sudan Kusini mjini Khartoum, Mayen Dut Wol, amesema bila kupata maelewano juu ya masuala hayo ya kiusalama, itakuwa vigumu kuyatekeleza mengine yatakayoafikiwa.

''Bila kufikia maelewano juu ya masuala ya kiusalama na mpaka, nina uhakika kwamba hata tukisaini makubaliano juu ya mafuta na mengine ya kiuchumi, utekelezaji wake utakuwa mgumu sana.'' Amesema Wol.

Abyei bado kikwazo

Kila upande unadai kuwa eneo la Abyei lenye mafuta ni lake
Kila upande unadai kuwa eneo la Abyei lenye mafuta ni lakePicha: Reuters

Umiliki wa jimbo linalozozaniwa la Abyei, na kutenga eneo lisilo na shughuli zozote za kijeshi kati ya Sudan na Sudan Kusini, ni miongoni mwa mada ngumu katika mkutano huo. Eneo hilo, linaweza kuukatiza msaada kwa waasi wa katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile, ambao Sudan inadai wanaungwa mkono na serikali ya mjini Juba.

Mikondo kadhaa ya mazungumzo kati ya nchi hizo mbili imekwishaambulia patupu, lakini sasa, kukutana ana kwa ana kwa marais wawili, na mbinyo wa Umoja wa Mataifa ambao unaambatana na kitisho cha kuziwekea nchi hizo vikwazo iwapo zitashindwa kuelewana, vimetoa matumaini mapya ya mafanikio.

Muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa Mataifa kwa marais wa nchi hizo kuelewana juu ya masuala ambayo hayakupatiwa ufumbuzi wakati Sudan ilipopata Uhuru wake Julai mwaka jana, ulimalizika Jumamosi iliyopita.

Muda huo uliwekwa baada ya makabiliano makali baina ya nchi hizo, baada ya jeshi la Sudan Kusini kulikalia kwa muda eneo lenye kuzalisha mafuta la Heglig, na Sudan kujibu kwa mashambulizi ya ndege za kivita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amewatolea wito marais Al-Bashir na Kiir kumaliza tofauti zao, ili mkutano huu wa kilele uweke kikomo kwenye kipindi cha mizozo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Josephat Charo