1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani nchini Zimbabwe yaanza leo mjini Pretoria

Nijimbere, Gregoire22 Julai 2008

Mazungumzo ya kusaka amani nchini Zimbabwe yanaanza leo mjini Pretoria, Afrika ya kusini, siku moja baada ya rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kusaini mkataba wa kuanza mazungumzo.

https://p.dw.com/p/EhSy
Rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan TsvangiraiPicha: AP

Mazungumzo hayo ambayo yatafanyika mjini Pretoria nchini Afrika ya kusini, yamepewa muda wa wiki mbili kufikia mwafaka. Afisa moja wa chama cha MDC cha Morgan Tsvangirai ambae hakutaka jina lake litajwe, amethibitisha kuwa wajumbe wa chama hicho wanasafiri leo kuelekea mjini Pretoria, tayari kwa mazungumzo hayo. Pande zote mbili zinasema zipo tayari kuzungumza. Rais Robert Mugabe amesema: ´´Lazima tufanye kitu. Ikiwa hatukuweza kufanya hapo kabla, sasa tufanye, tufikirie na tufanye kama wazimbabwe na tuwe waamuzi wa mstakabali wetu´´ Naye Morgan Tsvangirai, kiongozi wa upinzani, amesema wanaunganisha juhudi: ´´Tunaweka akili zetu pamoja. Naamini tunaweza kupata suluhu. Kwa hakika kukosa suluhu sio chaguo´´.

Rais wa Afrika ya kusini Thabo Mbeki mpatanishi katika mgogoro wa Zimbabwe kwa niaba ya jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, amesema kutakuwa na shughuli mfululizo ili kufikia suluhu haraka iwezekanavyo. Miongoni mwa yale yaliyomo katika mkataba wa kuanza mazungumzo uliyotiwa sahihi hapo jana mjini Harare kati ya rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai, hakuna kikao cha bunge wala cha serikali kitakachoitishwa wakati wa mazungumzo hayo, pande zote zikomeshe machafuko, na shughuli za kibinaadamu kuwasaidia wale wote waliolazimishwa na machafuko kuyahama maskani yao zianze mapema iwezekanavyo. Na miongoni mwa maswala yatakayozungumziwa, ni pamoja na pendekezo la kutunga katiba mpya, mageuzi ya idara za uongozi, mwingilio wa nchi za kigeni katika maswala ya ndani ya Zimbabwe, mageuzi ya kilimo na kuinua uchumi.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amekaribisha mkataba huo wa kuanza mazungumzo Zimbabwe na kuzisihi pande husika kufanya kila juhudi kufikia suluhu kuikwamua nchi kisiasa, kiuchumi na kibinaadamu. Umoja wa Afrika kupitia mkuu wa Halmashauri ya Umoja huo Jean Ping, umepongeza pande mbili Zimbabwe na kuzitaka zijenge juu ya msingi huo wa mkataba wa kuanza mazungumzo uliofikiwa hapo jana. Rashia imesema mkataba huo wa kuanza mazungumzo unaipa haki Rashia pale ilipopiga kura ya turufu pamoja na China kuzuwia azimio la vikwazo dhidi ya serikali ya Zimbabwe. Lakini Marekani haijaridhika kwani, pamoja na kuukaribisha mkataba huo wa kuanza mazungumzo, inaweka sharti mazungumzo hayo yaelekezwe kwenye matakwa ya raia. Umoja wa Ulaya umekwenda mbali zaidi kwa kukaza vikwazo dhidi ya serikali ya rais Robert Mugabe.