1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Ukraine kuendelea ?

26 Desemba 2014

Viongozi wa Ukraine na waasi wanoungwa mkono na Urusi, wanajaribu kufufuwa mazungumzo ya amani yaliyokwama kutokana na tafauti kubwa juu ya namna ya kumaliza vita vya waasi vya miezi minane.

https://p.dw.com/p/1EAMn
Balozi wa Ukraine nchini Belarus Mikhail Yezhel wa kwanza (kushoto) na Rais wa zamani wa Ukraine Leonid Kuchma wa pili (kushoto) wakiwa mjini Minsk. (24.12.2014)
Balozi wa Ukraine nchini Belarus Mikhail Yezhel wa kwanza (kushoto) na Rais wa zamani wa Ukraine Leonid Kuchma wa pili (kushoto) wakiwa mjini Minsk.( 24.12.2014)Picha: picture-alliance/dpa/Viktor Drachev

Mkutano uliokuwa na mvutano mkubwa chini ya upatanishi wa wajumbe kutoka Urusi na Ulaya uliofanyika katika mji mkuu wa Belarus hapo Jumatano ulikuwa ukitarajiwa kufuatiwa na mkutano wa mwisho Ijumaa (26.12.2012) ambapo makubaliano kamili ya amani yalitakiwa yasainiwe.

Lakini kikao cha Jumatano kilivunjika baada ya zaidi ya masaa matano kwa kufikiwa tu makubaliano juu ya suala ambalo halikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya vipengele vinne viliomo kwenye agenda nalo ni suala la kubadilishana wafungwa kutakakowahusisha wafungwa 250 wapiganaji waasi na wanajeshi 150 wa Ukraine.

Mabadilishano ya wafungwa yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kwa kuwahusisha wafungwa kadhaa.

Ukosefu wa kuaminiana

Imeonekana kwamba hawakuweza kujenga hali ya kuaminiana kati ya makundi hasimu kwenye mzozo huo kama vile ilivyokuwa imetarajiwa na mataifa ya magharibi.

Waandishi wa habari wakisubiri nje ya Kasri la Rais mjini Minsk kuanza mazungumzo ya amani ya Ukraine.(24.12.2014)
Waandishi wa habari wakisubiri nje ya Kasri la Rais mjini Minsk kuanza mazungumzo ya amani ya Ukraine.(24.12.2014)Picha: AFP/Getty Images/M. Malinovsky

Msemaji wa serikali ya Belarus, Dmitry Mironchik, ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kwamba "hakutakuwepo na mkutano wa kundi la mawasiliano linaloshughulikia mzozo huo wa Ukraine leo hii".Hata hiyo wawakilishi wa waasi na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE wamesema mkutano huo yumkini ukaendelea leo hii.

Msaidizi mmoja wa makundi mawili ya waasi amesema alikuwa anarudi katika jimbo la mashariki la waasi la Donetsk kwa sababu inaonekana kwamba hakuna faida ya kubakia Minsk.

Lakini duru ya ngazi ya juu ya Ukraine imeliambia shirika la habari la AFP kuna fursa ndogo kwamba mkutano huo wa Minsk utaweza kuandaliwa Ijumaa iwapo mashauriano zaidi ya awali yataendelea kufanyika.

Azma ya mazungumzo

Mazungumzo hayo yalikuwa yamekusudia kuyapa nguvu makubaliano mawili yaliofikiwa mwezi wa Septemba ambayo yalikuwa yamekusudia kukomesha mzozo huo wa umwagaji damu mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya kwa miaka mingi na kuidumisha Ukraine kuwa ni taifa moja wakati mikoa inayopakana na Urusi ikipatiwa mamlaka zaidi ya kujiendesha.

Makao makuu ya serikali mjini Minsk ambapo yanafanyika mazungumzo ya mani ya Ukraine.
Makao makuu ya serikali mjini Minsk ambapo yanafanyika mazungumzo ya mani ya Ukraine.Picha: picture-alliance/dpa/Viktor Drachev

Lakini ni masuala machache yalioafikiwa miezi minne iliyopita yameweza kufanikishwa. Mikoa yenye viwanda vikubwa ya Luhansk na Donetsk iliandaa chaguzi zao wenyewe za kuchaguwa viongozi hapo mwezi wa Novemba na kuighadhibisha serikali ya Ukraine pamoja na kuuwa matumaini ya kufikiwa kwa suluhisho la kisiasa katika kipindi cha karibuni.

Makamanda walioko kwenye medani za mapambano wa pande zote mbili ambao hawawajibiki kwa mtu yoyote wamekuwa wakiendelea kupuuza azimio rasmi la kusitisha mapigano na kuendeleza vita vilivyouwa zaidi ya watu 1,300.

Kazi nzito

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanahofu kwamba idadi yao ya jumla ya watu waliouwawa katika mapambano 4,700 yumkini ikawa kubwa zaidi kutokana na kwamba wanamgambo wamekuwa wakificha kiwango chao cha maafa na kuwazuwiya watu kutoka nje kufika kwenye maeneo ya makaburi.

Wanajeshi wa serikali Ukraine.
Wanajeshi wa serikali Ukraine.Picha: Reuters/G.Garanich

Jukumu gumu kabisa linalowakabili wapatanishi wa Umoja wa Ulaya litakuwa ni kutafuta njia ya kuzifanya pande hizo mbili zikubali kuanza kuvirudisha nyuma vifaru vyao ili kwamba kanda ya kuzuwiya mapambano ya kilomita 30 iweze kuanzishwa kwenye eneo la vita.

Waasi hivi sasa wana utashi mkubwa wa kutaka kuona kuanza tena kutolewa malipo ya ustawi wa jamii ambayo serikali ya Ukraine iliyazuwiya mwezi uliopita kwa kuhofia kwamba yalikuwa yakitumika kugharamia uasi. Kwa mujibu wa duru za mkutano wa Jumatano timu zilikuwa hazikuweza hata kukubaliana juu masuala gani yanayopaswa kujadiliwa.

Hawana weledi

Duru zilizo karibu na msimamo wa serikali ya Ukraine katika mazungumzo hayo zimewaita wajumbe wa waasi kuwa ni watu wasio na weledi kabisa ambao hawahusiki katika maamuzi na hawana wanachokijuwa juu ya makubaliano yaliyopita.

Waasi katika jimbo la Donetsk.
Waasi katika jimbo la Donetsk.Picha: picture-alliance/dpa/Alexey Kudenko

Duru hiyo imesisitiza kwamba iwapo wataendelea itapaswa tu kwa ajili ya kusaini makubaliano ya Minsk na kuyaendeleza zaidi na sio kuyachambuwa upya ambacho ndicho wanachojaribu kukifanya wawakilishi wa Luhansk na Donetsk.

Wapatanishi wa Ulaya na Urusi hadi sasa wamekaa kimya na kuwaachia mahasimu hao wawili watafute msimamo wa pamoja.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef