1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani yakwama tena.

25 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cfzf

Jerusalem.

Mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina yanayofanyika mjini Jerusalem yamekwama tena kutokana na kutokukubaliana baada ya Wapalestina kuondoa uwezekano wa kuendelea na mazungumzo hayo hadi pale Israel itakapokubali kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi. Wizara ya ujenzi ya Israel imefichua mpango wa ujenzi wa nyumba 500 katika eneo la Har Homa na nyumba 240 katika eneo la Maale Adumim karibu na Jerusalem mwakani.

Mpango huo umekosolewa na Marekani pamoja na umoja wa Ulaya. Kiongozi wa majadiliano hayo kutoka Palestina Ahmed Qurie amemwambia mwenzake wa Israel , waziri wa mambo ya kigeni Tzipi Livni , kuwa Israel inapaswa kuchagua baina ya njia kuelekea amani na majadiliano , ama njia ya ujenzi wa makaazi hayo. Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa Palestina Mahmoud Abbas watakutana baadaye wiki hii kujaribu kuyaokoa mazungumzo hayo yaliyoanzishwa katika mkutano wa amani wa Annapolis , Maryland nchini Marekani mwezi uliopita.