1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya COP23 yajadili bima dhidi ya majanga

Caro Robi
9 Novemba 2017

Wajumbe wanaohudhuria mkutano wa kimataifa wa mazingira Bonn, Ujerumani wamehimizwa kuunga mkono mipango ya kuwasaidia watu wanaopoteza mali zao kutokana na majanga kupata bima nafuu kuweza kuwalinda dhidi ya hasara.

https://p.dw.com/p/2nKlB
Äthiopien Gode - Dürre-Krise
Picha: DW/J. Jeffrey

Wajumbe wa mkutano wa mazingira wa COP23 wanahimizwa kuja na mawazo ya kupatikana suluhisho la kuwepo aina mbali mbali zitakazosaidia katika kupunguza hasara wanazopata watu hasa wa kutoka mataifa masikini wanaojikuta katika hatari ya kupoteza mali zao ikiwemo mifugo kutokana na kiangazi cha muda mrefu kinachosababisha ukame na hivyo kutokuwepo kwa lishe za mifugo wao.

Aidha, wanaojikuta wamebaki bila ya makazi au ardhi zao haziwezi kukalika tena au kutumika kwa ajili ya kilimo kutokana na mikasa kama mafuriko, mmonyoko mbaya wa udongo au maporomoko ya ardhi.

Majanga yanapotokea, mara nyingi yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kuwa na mbinu za kujikwamua kwa wakati ufaao ndiyo tofauti kati ya kujinusuru na kupoteza matumaini wakati mwingine ikiwa ndiyo tofauti kati ya uhai na mauti.

Majanga yasababisha umasikini usiokwisha

Katika nchi nyingi zinazoendelea, watu wengi masikini wa nchi hizo huwa hawana uwezo wa kuchukua bima kujilinda pamoja na mali zao dhidi ya majanga. Wanakosa raslimali zinazohitajika kuyajenga upya maisha yao na miundo mbinu na hivyo mkondo wa umasikini unaendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Sierra Leone Erdrutsch in Kamayama bei Freetown
Athari za maporomoko ya ardhi Sierra LeonePicha: DW/O. Acland

Ushirikiano wa kimataifa unaozijumuisha nchi saba zilizo na nguvu zaidi za kiuchumi G7, nchi ishirini zilizoendelea zaidi kiuchumi na zinazoinukia G20 na nchi 20 zilizo katika hatari zaidi zijulikanazo V20 zinachangia katika mpango huo ulioanzishwa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi wa kupataikana kwa bima nafuu kuwalinda watu, jamii na nchi dhidi ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Wataalamu wa mazingira wanaohudhuria mkutano huu wa COP23 wanajadili pia njia zinazoweza kutumika kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi. Wakati huo huo, wajumbe wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuhusu mageuzi muhimu kuhusu gesi ya Carbon.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo magumu miongoni  mwa nchi za umoja huo, bunge la Ulaya na halmashari ya Umoja wa Ulaya kuafikiana kuhusu mageuzi juu ya mfumo wa kibiashara wa kutolewa kwa gesi ya Carbon ujulikanao ETS utakaoanza kutumika baada ya mwaka 2020.

Annikky Lamp, msemaji wa Estonia, taifa ambalo kwa sasa ndilo linalokalia kiti cha urais wa Umoja wa Ulaya, amesema "matokeo ya makubaliano hayo muhimu yanaimarisha mfumo wa ETS, kudumisha heshima kwa mazingira na kusaidia ugunduzi na teknolojia mpya kwenye sekta ya nishati."

Mfumo huo unanuiwa kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani na kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia malengo yao ya kuyalinda mazingira kwa kupunguza gesi hiyo kutoka karibu viwanda 12,000.

 

Mwandishi: Caro Robi/unfcc/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef