1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kusaka amani Burundi yamalizika Arusha

Charles Ngereza29 Oktoba 2018

Hatua ya serikali ya Burundi kushindwa kushiriki katika mazungumzo hayo iliibua shutuma

https://p.dw.com/p/37KjN
Tansania - Burundi Friedensgespräche mit Benjamin Mkapa
Picha: Charles Ngereza

Mazungumzo ya awamu ya tano na ya mwisho kusaka amani nchini Burundi yamemalizika Jumatatu (29.10.2018) mjini Arusha Tanzania huku wajumbe wa mkutano huo wakiwa na wasiwasi wa kupatikana kwa amani ya taifa hilo kupitia mazungumzo hayo ambayo yamesusiwa na serikali ya Burundi  bila kutoa sababu yoyote.

Hatua ya serikali ya Burundi  kushindwa kuwasili Arusha mwanzoni mwa juma lililopita kushiriki katika mazungumzo hayo iliibua shutuma kali kutoka kwa msuluhishi na makundi yote yanayoyoshiriki mazungumzo hayo ambao kwa pamoja walilaani hatua hiyo wakisema inakwamisha jitihada za kupatikana kwa amani katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Wajumbe kutoka vyama vya siasa wa Burundi waliopo ndani na uhamishoni waliohudhuria mazungumzo hayo ya siku tano wamesema ingawa wametoa maoni na mapendekezo yanayofaa kumaliza mgogoro huo lakini hatua ya serikali kutoshiriki inaleta wasiwasi wa maoni yao kukubaliwa.

Msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Benjamin Mkapa ambaye pia ni rais wa zamani wa Tanzania
Msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Benjamin Mkapa ambaye pia ni rais wa zamani wa TanzaniaPicha: Charles Ngereza

Kiongozi wa chama cha Kaze FDD Jean Bosco Ndayikengurukie amesema serikali ya Pierre Nkurunziza inafanya makusudi kupoteza wakati hatua ambayo haivumiliki.

Naye Joseph Karumba mwanasiasa maarufu nchini Burundi hapa anaeleza sehemu ya mapendekezo waliyoyawasilisha kwa msuluhishi msaidizi wa mgogoro huo Benjamin  Mkapa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha CNDD Leonard Nyangoma anasema pamoja na kuwa wametoa mapendekezo ya jumla lakini anasema mazungumzo yajayo yafanyike katika ngazi ya umoja wa mataifa.

Balozi Kapya akizungumza kwa niaba ya msuluhishi wa mgogoro Burundi amesema kuwa msuluhishi amepokea mapendekezo ya wajumbe wote na baadaye ataandaa ripoti maalum atakayoiwasilisha kwa msuluhishi mkuu wa mgogoro huo Rais Yoweri Kaguta Mseveni ambaye naye ataiwasilisha katika mkutano wa wakuu wa  nchi za Afrika mashariki mwishoni mwa mwaka huu.

 

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman