1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuunda serikali yaanza Ujerumani

Admin.WagnerD23 Oktoba 2013

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Jumatano hii anazindua mazungumzo rasmi na chama kikuu cha upinzani cha Social Democrats SPD, yanayolenga kufikia muafaka wa kuunda serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/1A4sC
Kansela Angela Merkel na mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel.
Kansela Angela Merkel na mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel.Picha: picture-alliance/dpa

Muungano wa Merkel wa vyama vya CDU na CSU ulikubaliana kuundwa makundi 12 ya kikazi yatakayosaidia kuendesha mazungumzo hayo na kutafuta muafaka kati ya pande husika.

Pamoja na Merkel, wajumbe 75 wa ngazi za juu kutoka vyama hivyo vitatu watahudhuria duru ya ufunguzi wa mazungumzo hayo hii leo, akiwemo mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union CSU Horst Seehofer, na yule wa SPD Sigmar Gabriel.

Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akiteta na makatibu wakuu wa vyama vya CDU, CSU, baada ya ibada ya misa katika kanisa la Mt. Hedwig, kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kuunda serikali.
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel (wa pili kushoto), akiteta na makatibu wakuu wa vyama vya CDU, CSU, baada ya ibada ya misa katika kanisa la Mt. Hedwig, kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kuunda serikali.Picha: Getty Images

Hofu ya wanachama wa SPD
Ikiwa mazungumzo hayo yatafanikiwa, itakuwa mara ya tatu kwa Ujerumani kuongozwa na na muungano wa vyama vikubwa kabisa tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia. Lakini kabla SPD haijasaini makubaliano yatakayofikiwa, wanachama laki nne na 70 wa chama hicho laazima wayapigie kura makubaliano hayo.

Sehemu kubwa ya wanachama wa SPD wanasita kugawana madaraka na wahafidhina wa Merkel, baada ya kudidimia kwa umaarufu wa chama hicho kwa kiwango cha chini kabisa cha asilimia 23 katika uchaguzi wa mwaka 2009.

Masharti ya kujiunga na mazungumzo
Sharti muhimu la SPD kujiunga na muungano wa Merkel katika misingi ya serikali aliyoingoza kati ya mwaka 2005 na 2009, ni kuanzisha kima cha chini kitaifa cha mshahara wa euro 8 na senti 50 kwa saa.

Hata hivyo, SPD wamelegeza kamba katika suala ka kupandisha kodi kwa matajiri, katika matumaini ya kupata makubaliano na Merkel kuhusu kima cha chini cha mshahara, ingawa katibu mkuu wa chama hicho Andrea Nahles, anasema itakuwa vigumu kufadhili miradi ya maenedeleo bila kupandisha kodi.

"Bila shaka katika mazungumzo hayo tuhahitaji ufafanuzi juu ya namna ya kufadhili miradi ya maendeleo. Tumeskia mengi kuhusu kupandishwa kwa kodi katika wiki zilizopita, lakini hakuna maelezo ya namna kila kitu kitafadhiliwa pasipo kupandisha kodi, na hilo laazima litaletwa kwenye meza ya mazungumzo leo," alisema Nahles katika mahojiano na Televisheni ya umma, ARD.

Sigmar Gabriel na Kansela Merkel.
Sigmar Gabriel na Kansela Merkel.Picha: picture-alliance/dpa

SPD pia inapanga kumshikiza Kansela Merkel wakati wa mazungumzo hayo kukubali kuruhusu suala la uraia wa nchi mbili, na malipo sawa kwa wanawake, pamoja na hatua za kuboresha huduma za wazee, na uwekezaji zaidi katika miundombinu na elimu.

Kizingiti muhimu
Katibu mkuu wa CDU Hermann Groehe, alisema chama chake kinalenga kutumia majadiliano hayo kufikia makubaliano juu ya hatua za kuimarisha uchúmi na kutengeneza nafasi zaidi za ajira.

Wakati CDU imeashiria utayari wake wa kukubaliana na SPD kuhusu masuala muhimu, ni suala la kima cha chini cha mshahara linalotarajiwa kuwa kizingiti muhimu katika mazungumzo hayo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,rtre
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman