1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Mashriki ya Kati yameanza Washington

2 Septemba 2010

bibi Hillary Clinton awakaribisha rasmi wajumbe wa pande 2.

https://p.dw.com/p/P2qm
Netanyahu na Hillary ClintonPicha: AP

Waziri wa nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton,ameyafungua rasmi hivi punde katika wizara yake mjini Washington, mazungumzo kati ya viongozi wa Israel na wa Palestina, Netanyahu na Abbas. Bibi Clinton, alitoa pongezi na shukurani kwa rais Hosni Mubarak wa Misri ,waziri-mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na kundi lake la pande 4 juu ya Mashariki ya Kati pamoja na washirika waliowezesha mazungumzo haya kuanza tena.

Netanyahu, alimshukuru Bibi Clinton na Rais Obama kwa juhudi zao za kuleta amani ya kudumu Mashariki ya Kati.Alionya Netanyahu lakini, kufikia shabaha hiyo haitakua rahis. Nae Kiongozi wa Palestina,Mahmud Abbas, alitoa pia shukurani zake kwa Rais Obama, waziri wa nje Bibi Clinton,mjumbe wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Bw.Mitchel kwa kufufua mazungumzo haya juu ya maswali ya mwisho ya kufikia suluhu ya Mashariki ya Kati.

Swali nyeti linaloweza kuyachafua mazungumzo kabla ya hata hayakufika mbali, ni kuendelea ujenzi wa maskani za walowezi wa kiyahudi katika ardhi za wapalestina. Chama cha Hamas, kimeahidi kuyachafua mazungumzo kikidai kwamba, Mahmud Abbas,Kiongozi wa Palestina hana haki wala mamlaka ya kuwasemea wapalestina wote.

Rais Obama, amejitolea mno kusukuma mbele juhudu za kusaka amani kati ya Israel na wapalestina tangu kushika wadhifa wake wa urais huku akielewa heba yake yaweza ikaathirika katika uchaguzi wa Bunge-Congress hapo Novemba,mwaka huu iwapo mazungumzo haya yakienda kombo.Kwahivyo, alizitaka pande zote mbili kuitumia fursa hii.

"Kama nilivyomuambia kila mmoja wao hii leo, fursa hii, huenda isitokee tena karibuni.Hawamudu kuiacha iwaponyoke."-alisema Obama.

Waziri-mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akasema nae,

"Nimekuja hapa kusaka suluhu itakayoingia katika historia.Itakayo wawezesha watu wetu wa pande zote mbili kuishi kwa amani, usalama na kwa heshima na utu."

Akichangia Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya wa Palestina,Mahmud Abbas, alisema,

"Tutafanya kila tuwezalo na tutajitahidi sana, tena bila ya kuchoka, ili kuhakikisha kuwa, mazungumzo haya yanafikia shabaha yake -kutatua swali la Jeruselem na wakimbizi."

Wapinzani wa juhudi hizi za amani na mzungumzo haya pamoja na ridhaa zitakazo hitajika ili kufikia muafaka wanatishia kuyavuruga.

Huko Gaza,chama cha Hamas, chenye mamlaka katika mwambao huo, kimearifu kuwa, wanamgambo wake wataendelea kuhujumu maskani za walowezi wa kiyahudi katika ukingo wa Magharibi ambako polisi wa Palestina wamewatia mbaroni zaidi ya wafuasi 500 wa Hamas wakitiliwa shaka kuhusika na hujuma ya kuuwawa walowezi 4 wa kiyahudi hapo juzi.

"Mahmud Abbas, hana haki ya kuwasemea wapalestina"-alisema msemaji wa chama cha Hamas.

Nao walowezi wa kiyahudi wametangaza kwamba, wataendelea kujenga maskani zaidi haraka katika mitaa yao ya ukingo wa magharibi na hivyo kutojali mpango wa serikali ya Israel wa kusimamisha ujenzi kwa sasa.Wanapanga kujenga maskani 80 tena haraka.

Swali la ujenzi wa maskani ni nyeti kabisa na laweza kuyatia munda mazungumzo ya leo mjini Washington.Bw.Abbas ameonya kwamba atajitoa kwenye mazungumzo ikiwa Israel haitarefusha muda wa mpango wake wa kusimamisha ujenzi wa maskani unaomalizika Septemba 26 mwaka huu.

Tangu waziri mkuu Netanyahu hata Bw.Abbas, walionesha kutaka maafikiano baada ya mazungumzo yao ya jana na rais Obama lakini pia wote wawili walisisitiza maswali yao ya kimsingi:Usalama upande wa Israel kwa Bw.Netanyahu na harakati za ujenzi wa maskani upande wa Bw.Abbas.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed