1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia ya Iran yaanza leo

20 Novemba 2013

Mazungumzo magumu yanaanza leo kati ya Iran na mataifa makubwa kutafuta makubaliano kwa mpango wa nyuklia wa Iran ambayo pia yatawaridhisha wanasiasa wa msimamo mkali huko Marekani, Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

https://p.dw.com/p/1ALFJ
Catherine Ashton Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja (kushoto) na Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva baada ya kushindwa kufikiwa kwa makubaliano. (10.11.2013).
Catherine Ashton Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja (kushoto) na Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva baada ya kushindwa kufikiwa kwa makubaliano. (10.11.2013).Picha: Reuters/Jason Reed

Mazungumzo hayo yanafanyika Geneva wakati kukiwa na hali ya mvutano inayoongezeka Mashariki ya Kati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Iran akiishutumu Israel kwa kujaribu kuvuruga mchakato huo kufuatia mirupuko miwili ya mabomu iliouwa takriban watu 23 nje ya ubalozi wa Iran mjini Beirut hapo jana.Wizara ya mambo ya nje ya Iran imeilaumu Israel na mamluki wake kwa kuhusika na miripuko hiyo.

Israel imekanusha madai hayo na Waziri Mkuu wake Benjamin Netanyahu leo hii anatarajiwa kuendeleza kampeni yake dhidi ya kufikia makubaliano ya nyuklia na Iran wakati atakapokutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Moscow.

Iran ina matumaini

Iran Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif ameonekana kutokata tamaa kuhusu nafasi za kufikiwa kwa makubaliano mjini Geneva ikiwa ni siku 10 baada ya mazungumzo kati ya Iran kwa upande mmoja na kwa upande wa pili Marekani, China, Urusi, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kushindwa kufikia makubaliano.Amekaririwa akisema kwamba anadhani kuna kila uwezekano wa mafanikio.

Lakini Rais Barack Obama wa Marekani ambaye amekuwa akiwashawishi wabunge wa Marekani kutoiwekea vikwazo zaidi Iran ameonekana kuwa na msimamo wa hadhari zaidi juu ya uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano na mapema. amekaririwa akisema "Hatujuwi iwapo tutaweza kufikia makubaliano na Iran wiki hii au wiki ijayo."

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Wabunge wa Marekani hapo jana wameitaka serikali ya Marekani iwe na msimamo mkali katika mazungumzo yake na Iran kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ilisema jana kwamba waziri mkuu huyo pia alizungumza kwa simu na Rais Hassan Rouhani wa Iran ambayo yalikuwa ni mawasiliano ya kwanza kati ya viongozi wa nchi hiyo katika kipindi cha muongo mzima na viongozi hao wamekubali kwamba ni muhimu kuitumia fursa iliopo.

Vitisho na vikwazo vikomeshwe

Shirika la habari la serikali la Iran IRNA limemkariri Rouhani akimwambia Cameron kwamba nchi hiyo imeazimia kuhakikisha kwamba shughuli zake za nyuklia zinaendelea kwa ajili ya matumizi ya amani na itatetea kwa nguvu haki zake za nyuklia. Ameongeza kusema hawatokubali ubaguzi katika suala hilo na kwamba lugha ya heshima lazima ichukuwe nafasi ya ile ya vitisho na vikwazo.

Rais Hassan Rouhani wa Iran.
Rais Hassan Rouhani wa Iran.Picha: picture alliance/Newscom

Mataifa makubwa yanataka kufikiwa kwa makubaliano ya awamu ya kwanza ambapo kwayo Iran inatakiwa isitishe sehemu ya shughuli zake nyeti kabisa za nyuklia wakati makubaliano ya muda mrefu yakiandaliwa.Lakini suala ni iwapo Iran yenye kupigania kuregezwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa,Marekani na Umoja wa Ulaya ambavyo vimeathiri sana usafirishaji nje wa mafuta ya nchi hiyo itakubali kile kinachopendekezwa badala yake.

Wataalamu wanasema iwapo haiba ya uchangamfu anayoitumia Rais Rouhani kuwasiliana na mataifa ya magharibi itashindwa kuupatia ufumbuzi mzozo wa nyuklia wa nchi hiyo atakuwa katika hatari ya kuacha kuungwa mkono na kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ali Khamenei ambaye leo amesema mataifa ya magharibi lazima yaheshimu mistari mekundu ya nchi hiyo na pia kuitaka serikali ya Iran kuheshimu mistari hiyo na kutotiwa kiherehere na makelele ya maadui na wale walioko dhidi ya Iran.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman