1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya pande sita yaanza Beijing.

Nyanza, Halima10 Julai 2008

Mkutano wa viongozi wa ujumbe wa mazungumzo ya pande sita kuhusu kukomesha shughuli za nyuklia za Korea Kaskazini, umefunguliwa leo Beijing, China baada ya kukwama kwa miezi tisa.

https://p.dw.com/p/Ea3W
Mtambo wa Yongbyon Korea kaskazini, ambao ulikuwa ni wa kwanza kwa nchi hiyo kutumia kufanyia jaribio lake la kwanza la nyuklia.Picha: AP


Wajumbe kutoka mataifa sita, wanaoshiriki mazungumzo hayo ya muda mrefu, wanakutana katika juhudi za kufanikisha suala hilo na kwamba yanafanyika baada ya Korea ya Kaskazini kuikabidhi China hati ya tathmini ya shughuli zake za nyuklia na kuteketeza kinu chake muhimu cha kurutubisha madini ya uranium mwezi uliopita.

Wajumbe hao pia wanazungumzia juu ya hatua nyingine zinazotakiwa katika utaratibu mzima wa kukomesha shughuli za kinyuklia za Korea ya kaskazini.

Mwenyekiti wa awamu hiyo ya mazungumzo, ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa China Wu Dawei amesema, mkutano huo ni jambo muhimu linalohimiza mazungumzo hayo kuingia kwenye kipindi kipya, lengo likiwa ni kupata maafikiano kwa mujibu wa matarajio ya pande mbalimbali, na kuyafanya maombi mapya ya pande hizo kuwa nguvu mpya ya kuhimiza mazungumzo, utekelezaji wa mpango wa kipindi cha pili na kuhimiza mazungumzo ya pande sita yaingie kwenye kipindi kipya.

Hata hivyo wajumbe kutoka Marekani na Korea Kusini, wameonya kuwa, hakutakuwa na maendeleo ya haraka ili kuweza kufikia lengo la Korea kaskazini, kuachana kabisa na mipango yake ya nyuklia ambayo imechukua muda mrefu kuutayarisha.

Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo hayo Christopher Hill, amesema kwa sasa wanalifanyia kazi tangazo hilo la Korea kaskazini.

Mazungumzo hayo ambayo yalianza mwaka 2003 na kuhusisha China, Korea kusini na Kaskazini, Marekani Japan na Urusi yalikwama kwa kipindi cha takriban miezi tisa kutokana na kutotolewa kwa tangazo la Korea Kaskazini kuhusiana na mradi wake huo wa nyuklia.

Lakini baada ya Koreka kaskazini kukabidhi tangazo hilo, Marekani ilijibu haraka kwa kuiondoshea nchi hiyo vikwazo vya biashara kama ilivyo afikiwa na mataifa hayo sita, Februari mwaka uliopita.

Aidha ikiwa ni sehemu ya mapatano hayo Marekani pia ilianza kuitoa Korea Kaskazini nchi ambayo Rais George W Bush aliwahi kuielezea kuwa ni moja wapo ya mihimili ya maovu duniani, katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi.

Tangazo hilo lililokabidhiwa China na Korea Kaskazini lilikuwa ni sehemu muhimu ya kile kilichoitwa awamu ya pili ya mapatano ya mwaka jana ya nchi hiyo kupunguza silaha, huku awamu ya kwanza ikiwa Korea Kaskazini inafunga kinu chake cha kurutubisha madini ya Plutonium kilichoko Yongbyon, Julai mwaka jana.

Chini ya usimamizi wa Marekani, Korea Kaskazini ilianza kuharibu kinu chake mwezi Novemba na kwamba mwezi uliopita ikalipua mnara wake wa kupoozea kinu hicho huko YongByon katika hali ya kuonesha dhamira yake ya kuachana na silaha za nyuklia.

Mtambo wa Yong byon ulikuwa ni nyenzo ya kwanza ya Korea kaskazini kutumia kufanya jaribio lake la kwanza la nyuklia.