1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Syria yaanza Geneva

Mohammed Khelef14 Machi 2016

Mazungumzo ya kusaka amani ya Syria yameanza mjini Geneva chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, huku ajenda za uundwaji wa serikali mpya, katiba na uchaguzi zikiwa juu ya meza.

https://p.dw.com/p/1ICvg
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura.Picha: Reuters/R. Sprich

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura, ameyaanza mazungumzo hayo kwa kutoa onyo kali kwa pande zote zinazoshiriki akisema kwamba huu unatakiwa uwe wakati wa kuambiana ukweli, akisisitiza kuwa hakutakuwa na Mpango B zaidi ya kurejea kwenye vita.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuyafungua mazungumzo hayo mchana wa leo mjini Geneva, de Mistura alisema endapo wawakilishi wa serikali na wa upinzani watashindwa kufikia makubaliano, basi suala hilo litarejeshwa kwa wale wenye ushawishi katika mazungumzo hayo ya amani, akimaanisha Urusi, Marekani, Kundi la Kimataifa la Kuisadia Syria na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Agenda imeshawekwa, inatokana na Azimio 2254 na ndani ya muundo na muongozo wa makubaliano ya Geneva. Wachafuzi watajaribu kutuparaganya kwa matukio mbalimbali lakini ataitwa na kuwajibishwa na jumuiya ya kimataifa na wale wote ambao nimewataja wenye uwezo wa aina hiyo," alisema de Mistura.

Serikali ya Assad yawasilisha mapendekezo

Katika hatua ya awali ya duru hii ya mazungumzo, pande hasimu hazikukutana, lakini serikali ya Rais Bashar al-Assad iliwasilisha waraka wake wa mageuzi ya kisiasa, huku balozi wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, akisema kuwa mazungumzo yake na de Mistura yalikuwa mazuri.

Kwa mujibu wa de Mistura, kamati mbili tafauti za mazungumzo hayo zitakuwa zinakutana sasa, moja inayohusiana na msaada wa kibinaadamu na nyengine juu ya usitishaji wa uhasama, huku msisitizo ukiwekwa kwenye suluhisho la kuwa na kipindi cha mpito cha utawala.

Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari.
Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari.Picha: Getty Images

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alisema katika siku hii ya kwanza kabisa, kila upande ulikuwa na kauli kali dhidi ya mwengine, lakini kwa ujumla wameonesha dhamira ya kusonga mbele.

Mapema, akiwa ziarani nchini Tunisia, waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alitoa wito kwa wapinzani na serikali kutokutumia vyombo vya habari kuumbuana.

"Tunatoa wito kwa pande zote kuepuka mitafaruku na mapambano kupitia vyombo vya habari na kukaa kitako wajadiliane kwa kusaka suluhu kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Pande husika nchini Syria zimekubali kwa mdogo uamuzi huo na kuahidi kuutekeleza."

Waangalizi wengi wanasema mazungumzo haya ni nafasi ya aina yake kupatikana kwa miaka kadhaa kuweza kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoingia mwaka wake wa sita sasa, vikiwa vimeshaangamiza maisha ya watu robo milioni, kuwachawanya wengine milioni 11 kama wakimbizi kwenye mataifa jirani na ndani ya nchi hiyo, na kutoa nafasi ya kukua na kusambaa kwa makundi ya kigaidi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman