1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbeki na juhudi za kusaka amani Sudan

25 Februari 2014

Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Sudan,Thabo Mbeki anafanya ziara mjini Khartoum akiwa na lengo la kusaidia kutia msukumo katika juhudi za kutafuta amani kati ya serikali ya Sudan na SPLM-N.

https://p.dw.com/p/1BF7F
Rais Salva Kiir,waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ba mpatanishi Thabo Mbeki
Rais Salva Kiir,waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ba mpatanishi Thabo MbekiPicha: Jenny Vaughan/AFP/Getty Images

Ziara hiyo ya Mbeki inafanyika kabla ya mazungumzo yanayotarajiwa kuanza tena mjini Ethiopia siku ya Ijumaa 28.02.2014.

Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan Thabo Mbeki anaianza ziara yake hiyo ya mjini Khartoum ikiwa tayari serikali ya Sudan na waasi wa Kordofan Kusini wameridhia kusitisha mapigano na kuruhusu msaada kuwafikia zaidi ya watu milioni 1 kwa mujibu wa makubaliano yaliyopendekezwa kabla ya kuvunjika mazungumzo ya kusaka amani wiki iliyopita.Itakumbukwa kwamba katika mkutano huo wiki iliyopita,wajumbe wa Umoja wa Afrika waliwasilisha pendekezo hilo kwa serikali ya Khartoum na waasi hao wa kundi la SPLM-N kabla ya mazungumzo hayo ya mjini Adis Ababa kuakhirishwa kutokana na pande hizo mbili kutupiana lawama.

Mwanajeshi wa Kundi la vuguvugu la ukombozi wa Sudan Kusini SPLM-N
Mwanajeshi wa Kundi la vuguvugu la ukombozi wa Sudan Kusini SPLM-NPicha: DW

Mpatanishi mkuu,wiki iliyopita alisema wajumbe kutoka upande wa waasi na serikali watabidi kushauriana na kundi la wapatanishi kuhusiana na mapendekezo hayo ya Umoja wa Afrika ingawa pia hakutowa maelezo zaidi kuhusiana na suala hilo. Kimsingi sasa mazungumzo hayo yanasubiriwa kuanza tena tarehe 28 mwezi huu wa Februari. Katika kikao cha mwanzo mjini Adis mkuu wa ujumbe wa waasi Yassir Armen alisema serikali ya Sudan inataka kumaliza vita hivi bila ya kutowa suluhisho katika suala zima la hali ya kibinadamu na kisiasa.

b#bKwa upande wake serikali ya Khartoum inalishutumu kundi hilo la waasi wa SPLM-N kwa kuongeza masuala ambayo hayahusiani na migogoro ya Kordofan Kusini na jimbo la Blue Nile. Mgogoro na uhasama wa kikabila katika majimbo hayo mawili pamoja na uasi wa muda mrefu katika jimbo la Darfur yametokana na malalamiko ya kiuchumi pamoja na kutengwa kisiasa kwa majimbo hayo na utawala wa Khartoum unaohodhiwa na waarabu.

Ni kutokana na hali hii rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye sasa ni mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika katika mzozo huu anataka kuzipa msukumo juhudi za kupatikana mwafaka wa amani baina ya pande hizo mbili zinazozana huku pia ukitarajiwa kufanyika mkutano wa tume ya pamoja ya Kimataifa iliyoundwa chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2011 kati ya Khartoum na muungano wa makundi ya waasi yaliyojitenga.Tume hiyo ilipewa jukumu la kufuatilia maendeleo ya makubaliano hayo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman