1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbio za ubingwa kati ya BVB na Bayern ni kali

Sekione Kitojo
28 Januari 2019

Mbio za kuelekea  ubingwa  katika  Bundesliga  nchini Ujerumani, zaongezeka  kasi  wakati  Borussia  Dortmund  na  Bayern  Munich zikifukuzana., na kuleta msisimko mkubwa kwa mashabiki.

https://p.dw.com/p/3CKWt
Fußball Bundesliga | Borussia Dortmund - Hannover 96 | Achraf Hakimi und Marco Reus
Picha: picture-alliance/nordphoto/Rauch

Mbio  za  kuelekea  katika  ubingwa  zimeanza  kushika  kasi mapema  msimu  huu , wakati  timu  mbili zilizoko  juu  ya  msimamo wa  ligi, zikionesha  nia  yake  ya  kunyakua  ubingwa  huo. Mabingwa  mara  sita  mfululizo  katika  Bundesliga  Bayern  Munich baada  ya  kuonekana  kuwa  haina  mshindani  katika  ligi  hii, mara hii imeachwa  nyuma  na  Borussia  Dortmund  katika  mchezo  wa 19  wa  Bundesliga, wakati  BVB  ikiwa  mbele  kwa  pointi  sita.

Fußball Bundesliga | 19. Spieltag | FC Bayern München - VfB Stuttgart
Wachezaji wa Bayern Munich Picha: picture-alliance/Fotostand/Wagner

Bayern Munich  ilihakikisha  mwanya  huo  hauongezeki  kuwa  pointi tisa, pale  ilipofanikiwa  kuikandika  VFB Stuttgart  kwa  mabao 4-1 jana  Jumapili, hali  ambayo  inafanya  mbio  hizo  kuwa  za kusisimua  zaidi.

Wakati  BVB inasema  haina  presha  kushinda  taji  hilo  msimu  huu, Bayern  ina  nia  ya  kuonesha  kwamba  wao  ni  miamba wasioshindika na  wanataka  kulinyakua  taji  hilo. Borussia Dortmund  ilichambua  kama  karanga  Hannover 96  kwa  kuishindilia mabao 5-1  siku  ya  Jumamosi, hali  inayoonekana  kuwa  kikosi hicho  cha  kocha  Lucien Favre  kina  nia  pia  kulinyakua  taji  hilo.

Thomas Doll kocha  mpya

Mambo  hayakuishia  hapo  baada  ya  kipigo  hicho Hannover 96 iliyoko  katika  hatari  ya  kushuka  daraja  iliamua  kuachana  na kocha  wake Andre Breitenreiter , na  kumteua Thomas Doll  kuwa mrithi  wake  katika  juhudi  za  kuiokoa  timu  hiyo kushuka  daraja msimu  huu. Kipigo  dhidi  ya  Dortmund  siku  ya  Jumamosi  kilikuwa cha  tatu  mfululizo, ikibakia  katika  pointi 11  na  katika  nafasi  ya 17 sawa  na  timu  iliyoko  mkiani  ya  Nuremberg.

Ferencvaros Budapest Thomas Doll press conference
Kocha mpya wa Hannover 96 Thomas DollPicha: picture alliance/dpa/F.Demir

Doll  ametia  saini  kuifunza  timu  hiyo  hadi  mwaka  2020, mkataba ambao  utadumu  hata  katika  daraja  la  pili  iwapo timu  hiyo itashuka  darja. Doll  mwenye  umri  wa  miaka 52 mchezaji  wa zamani  wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani, ambaye aliwahi  kuzifunza Hamburg SV  na  Borussia  Dortmund  katika  Bundesliga, katika miaka  ya  hivi  karibuni  aliwahi  kufunza  timu nchini  Saudi Arabia, Uturuki  na  Hungary.

Bayern Munich imejiimarisha  katika  nafasi  ya  pili ikiwa  na  pointi 42 , sita  nyuma  ya  Borussia  Dortmund. Wakati  nafasi  ya  tatu inashikiliwa  na  Borussia Moenchengladbach  ikiwa  na  pointi  39, ikifuatiwa  na  RB Leipzig  katika  nafasi  ya  nne  ikiwa  na  pointi 34, baada  ya  jana  Jumapili  kuirarua  Fortuna Dusseldorf  kwa mabao 4-0.

Fußball Bundesliga | 19. Spieltag | Fortuna Düsseldorf - RB Leipzig | Jubel (0:1)
Wachezaji wa RB Leipzig wakipongezana baada ya kupata bao dhidi ya Fortuna DusseldorfPicha: picture-alliance/dpa/M. Becker

Bayern wamhitaji mchezaji wa  Chelsea

Callum Hudson-Odoi  wa  Chelsea  hajaweka  wazi  hatima  yake baada ya  ripoti zilizozagaa  katika  vyombo  vya  habari  kwamba kijana  huyo  mshambuliaji  wa  pembeni  kuwasilisha  barua  yake ya  ombi  la  kutaka  kuihama  klabu  hiyo  kwa  viongozi  wake. Kijana  huyo  machachari  mwenye  umri  wa  miaka  18  alifunga bao  la  pili  wakati  mabingwa  wa  kombe  la  FA  nchini  England Chelsea  kuishinda  Sheffield  Wednesday  kwa  mabao 3-0  katika duru  ya  nne  ya  kombe  hilo  katika  uwanja  wa  Stamford Bridge jana  Jumapili.

Fußball England Tottenham Hotspur v Chelsea - Carabao Cup Semi- Final 1st Leg
Callum Hudson-OdoiPicha: picture-alliance/NurPhoto

Hudson-Odoi  hapo  kabla  alihusishwa  na  kuhamia  katika  klabu ya  Bayern  Munich, ambao  walisema  wazi  jinsi  wanavyomuhitaji kijana  huyo  anayeichezea  timu  ya  vijana  ya  England.

Alipoulizwa  baada  ya  mchezo  huo  kwamba  huenda  alicheza mchezo  wake  wa  mwisho na  Chelsea , Hudson-Odoi  aliiambia BBC , "Sifahamu, siwezi  kusema. Naendelea  kufanyakazi kwa nguvu  na  huwezi  kujua  kile  kitakachotokea."

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe, rtre, dpa , ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo