1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbivu na mbichi kujulikana leo Tanzania

25 Oktoba 2015

Wapigakura nchini Tanzania wanateremka vituoni kumchagua rais wa awamu ya tano pamoja na wabunge na madiwani, katika uchaguzi unaotazamiwa kuwa wa ushindani zaidi katika historia ya taifa hilo.

https://p.dw.com/p/1GtpT
Moja Kati ya Edward Lowassa (kushoto) kutoka Chadema, na John Pombe Magufuli (kulia) kutoka CCM ndiye atakuwa rais ajaye wa Tanzania.
Moja Kati ya Edward Lowassa (kushoto) kutoka Chadema, na John Pombe Magufuli (kulia) kutoka CCM ndiye atakuwa rais ajaye wa Tanzania.Picha: picture-alliance/AP Photo/Getty Images/AFP/DW Montage

Wagombea wakuu katika uchaguzi huu walihitimisha kampeni zao siku ya Jumamosi kwa nyimbo na densi katika mikutano mikubwa, ambapo chama tawala na upinzani waliahidi kuwaondoa mamilioni ya Watanzania kutoka katika umaskini na kukomesha rushwa.

Chama tawala - chama cha Mapinduzi kilichokaa madarakani tangu uhuru mwaka 1961, kinakabiliwa na ushindani mkali zaidi katika kipindi cha zaidi ya nusu karne, katika uchaguzi huu wa rais na wabunge.

Rais Jakaya Kikwete akimnadi mgombea wa chama chake Dk. John Pombe Magufuli.
Rais Jakaya Kikwete akimnadi mgombea wa chama chake Dk. John Pombe Magufuli.Picha: Getty Images/AFP/Stringer

Tafiti mbili kubwa za maoni zimembashiria ushindi John Magufuli, mgombea wa CCM, lakini wengi wantarajia chama hicho tawala kupoteza viti vingi vya ubunge, baada ya upinzani kuungana nyuma ya mgombea mmoja, Edward Lowassa.

Kampeni za uchaguzi huu zimeonyesha kuvunjwa moyo kwa umma na kasi ya mabadiliko katika taifa hilo lililojaaliwa rasilimali za gesi asilia na madini, lakini likiendelea kusalia nyuma ya mataifa mengine ya Afrika mashariki kimaendeleo.

Akihitimisha kampeni zake jijini Dar es Salaam jana, mgombea wa muungano wa vyama vikuu vya upinzani Edward Lowassa, alisema ni aibu kwa Tanzania kuendelea kuwa maskini miaka 54 baada ya uhuru, na kuwaomba wapigakura wampe ridhaa aweze kuitoa nchi hiyo katika hali ya kuwa ombaomba na kujitegemea.

Magufuli naye ni mabadiliko

Magufuli, waziri wa ujenzi wa sasa, pia amejinadi kama mgombea wa mabadiliko na hata kukosoa kasi ndogo ya maendeleo ya serikali inayomaliza muda wake ya rais Jakaya Kikwete, ambaye atastaafu baada ya kumaliza mihula yake miwili madarakani.

Mgombea wa Ukawa Edward Lowassa ameahidi kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya neema badala ya kuendela kuombaomba.
Mgombea wa Ukawa Edward Lowassa ameahidi kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya neema badala ya kuendela kuombaomba.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Katika Mkutano wake wa mwisho mkoani Mwanza, umbali wa karibu kilomita 1,100 kaskazini-mashariki mwa jiji la Dar es Salaam, Magufuli aliahidi kukomesha matatizo yasiyokwisha ya mgao wa umeme unaokwamisha biashara na kutumia hifadhi kubwa ya gesi iliyogunduliwa hivi karibuni nchini humo kukuza ajira katika taifa hilo.

Magufuli ambaye aliimba na kucheza baada ya mkutano wake wa Mwanza, amejionyesha kuwa mwanasiasa asiye na mzaha na ambaye anahakikisha mambo yanafanyika. Wafuasi wake wanamuita 'Tingatinga', baada ya mgombea huyo mwenye umri wa miaka 55 kujijengea sifa ya kujenga miundombinu inayohitajika sana ya barabara katika maeneo tofauti ya nchi.

Lowassa mwenye umri wa miaka 62, na waziri mkuu wa zamani anaeongoza upinzani, alijitoa katika chama tawala mwezi Julai baada ya chama hicho kukata jina lake katika ngazi ya kura za kutafuta mgombea wa kupeperusha bendera ya chama.

Rais ajaye atakabiliwa na changamoto kuu za kupunguza viwango vya juu vya umaskini, kufanya kazi ya ziada kuvutia uwekezaji, na kuondoa ukiritimba unaotajwa kuwa kikwazo cha maendeleo.

Mchuano mkali CCM, CUF Zanzibar

Katika visiwa vya zanzibar vyenye mamlaka ya kujitawala, raia pia wanapiga kura kumchaguwa rais wa Jamhuri ya Muungano. Lakini Wazanzibari wamejielekeza zaidi kwenye kinyanganyiro cha rais wa visiwa vyao, ambacho kinashirikisha wagombea 14.

Rais Ali Mohamed Shein anakabana koo na makamu wake Maalim Seif Sharif Hamad kutoka chama cha CUF Zanzbar.
Rais Ali Mohamed Shein anakabana koo na makamu wake Maalim Seif Sharif Hamad kutoka chama cha CUF.Picha: DW/M. Khelef

Rais pamoja na makamu wa kwanza wa rais wa visiwa hivyo -- wanaoongoza katika serikali ya umoja wa kitaifa, ndiyo wagombea wenye nafasi ya juu katika kinyanganyiro hicho kitakachowahusisha wapigakura 500,000 waliojiandikisha.

Wagombea wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda ni rais alieko madarakani Ali Mohamed Shein wa chama tawala CCM, daktari mwenye umri wa miaka 67. Anakabiliana na makamu wake wa rais Seif Sharif Hamad kutoka chama cha upinzani - chama cha wananchi CUF, anaewania nafasi hiyo ya juu kabisaa visiwani kwa mara ya tano.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.
Mhariri: Abdul Mtullya