1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbwa 46 waokolewa Korea Kusini

27 Machi 2017

Mbwa 46 wamesafirishwa hadi New York nchini Marekani kutoka Korea Kusini baada ya kuokolewa katika shamba moja ambako walikuwa wachinjwe kwa ajili ya kuliwa na binadamu.

https://p.dw.com/p/2a35h
Fluoreszierende Hunde in Südkorea
Picha: AP

Kwa mujibu wa taarifa ya wanaharakati wa Shirika la Kimataifa linalotetea haki za wanyama iliyotolewa siku ya Jumapili. (26.03.2017) mbwa hao walibahatika kukwepa ghadhabu ya kisu kutokana na juhudi za wanaharakati wanaotetea haki za wanyama.

Shirika hilo ndilo lililowaokoa mbwa hao ambao walikuwa hawalishwi chakula cha kutosha. Wanyama hao waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kennedy International Jumamosi jioni na kupelekwa katika makazi ya dharura huko New York, Maryland na Pennsylvania.

Shamba walikookolewa mbwa hao katika mji wa Goyang, kaskazini mwa mji mkuu Seoul, lilikuwa kama ghala lenye mwangaza kidogo mno na hewa chache sana, kiasi kwamba harufu ya amonia ingesababisha machozi kutoka machoni wakati mtu anapopitia hapo," alisema Kelly O'Meara, anayesimamia miradi ya kimataifa inayohusu wanyama. "Ungeona macho yanakuangalia lakini hungeweza kuwaona mbwa wenyewe gizani," aliongeza kusema.

O'meara pia alisema mashamba mengine ya aina hiyo yapatayo 17,000 bado yanaendesha shughuli zao Korea Kusini. Hata hivyo sekta hiyo inafifia katika jamii ambayo mahitaji ya nyama ya mbwa yamekuwa yakipungua kwa kiwango kikubwa, ingawaje nyama kutoka kwa mbwa milioni mbili bado inaliwa kila mwaka nchini humo.

Hundefleisch Restaurant in Südkorea
Mgahawa wa Daegyo mjini Seoul, Korea Kusini, unaouza nyama ya mbwaPicha: picture-alliance/AP Photo

Nchini Marekani mbwa hao waliookolewa wataweza kuasiliwa baada ya maafisa wa nyumba watakakokaa kutathmini tabia yao na mahitaji ya kimatibabu na kuhakikisha kila mmoja wao yuko tayari kwa ajili ya maisha mapya katika nyumba ya mtu fulani. O'meara  alisema huko Korea Kaskazini mbwa hawapewi matibabu ya aina yoyote ile. "Wanalazimika kuishi hivyo au wafe katika kizimba na wanapewa chakula cha kuwawezesha kuishi tu basi."

Shirika la kimataifa la kutetea haki za wanyama liliwaokoa mbwa zaidi ya 800 katika mashamba saba mnamo mwaka 2015 waliotakiwa kuchinjwa. Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Washington hutegemea michango binafsi, hufanya kazi moja kwa moja na wakulima kufunga na kuitokomeza biashara ya nyama ya mbwa na kuwasaidia kifedha wamiliki kufanya kazi nyingine mbadala.

O'meara alisema mbwa hao lazima wasafirishwe ng'ambo kwa sababu kwa ujumla hawatakikani Korea Kusini kama wanyama wa kufugwa majumbani au rafiki wa binadamu. Baadhi yao walikuwa wametelekezwa na wengine walifugwa ili wauzwe kama wanyama wa kufuga nyumbani, lakini kawaida ikishindikana basi hukabidhiwa kwa sekta ya nyama.

Mwandishi:Josephat Charo/ape

Mhariri:Yusuf Saumu