1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa amani Mashariki ya Kati

Thelma Mwadzaya19 Machi 2010

Kundi la kimataifa linaloushughulikia mzozo wa Mashariki ya Kati, maarufu Quartet, limeitolea Israel wito wa kusitisha ujenzi wa aina yoyote ile wa makazi ya walowezi.

https://p.dw.com/p/MXNp
Viongozi wa mazungumzo ya pande nne,Quartet:Tony Blair,Hillary Clinton, Sergey Lavrov,Ban Ki-moon na Catherine AshtonPicha: AP

Wanadiplomasia hao wa Umoja wa Mataifa, Marekani, Umoja wa Ulaya na Urusi wanaendelea na mkutano wao mjini Moscow,Urusi, ulio na azma ya kuishinikiza Israel hasa baada ya kutangaza kuwa itaanza ujenzi wa makazi mengine 1600 ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Jerusalem mashariki lililo na Waarabu wengi. Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisisitiza kuwa dhamira  yao ni  kuhakikisha kuwa wahusika wa mzozo huo wanarejea katika meza ya mazungumzo,''Sote tulikubaliana na tukasema kuwa kila mmoja wetu atatumia mbinu yoyote ile kufanikisha juhudi za kuwaleta pamoja wawakilishi wa Israel na Palestina katika meza ya mazungumzo. Kauli za leo zinaipa umuhimu mkubwa hatua ya kufikia makubaliano na amani ya eneo zima.'' alifafanua.

Pande nne

Mkutano huo, uliofanyika katika makazi ya Wizara ya mambo ya nje ya Urusi, uliwaleta pamoja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Mwakilishi wa pande nne wa mzozo  wa mashariki ya Kati, Tony Blair, Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, na mwenyeji wao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov. Kuhusu juhudi za wawakilishi wa mazungumzo hayo ya  pande nne, Waziri wa Mambo ya  Nje wa marekani, Hillary Clinton, alifafanua kuwa ,''Lengo la mazungumzo ya pande nne kama lile la serikali ya Marekani ni kuyafufua mazungumzo  hayo. Kamwe hatudhani kuwa mivutano ya pande zote ina manufaa yoyote na hilo tumeliweka bayana. Sote tumelilaani tangazo la Israel na tunataraji kuwa pande zote mbili zitarejea kwenye meza ya mazungumzo ya amani na  watazifanikisha harakati hizo kwa manufaa ya wote.'' katika kikao hicho.

NO-FLASH Israel erwidert Raketenangriff
Moshi uliotanda kusini mwa Ukanda wa Gaza baada ya shambulio la kombora la IsraelPicha: picture alliance/dpa

Vurugu za kidiplomasia?

Tangazo hilo la Israel la kuanza ujenzi wa makazi mapya liliwafanya Wapalestina kutoa wito wa kuyasitisha mazungumzo hayo kwa muda. Hatua hiyo, huenda ikauvuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Marekani iliyo msatari wa mbele kuhakikisha kuwa mwafaka unafikiwa. Israel, kwa upande wake, inaripotiwa kuwa imetoa taarifa iliyotokea afisi ya Waziri Mkuu  Netanyahu inayoashiria kuwa kutakuwa na ushirikiano wa aina fulani ndipo pande zote ziaminiane. Hata hivyo, maelezo kamili hayajabainika. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Ukanda wa Gaza inayozidi kuwa mbaya,''Tunatiwa wasiwasi mkubwa na hali katika Ukanda wa Gaza inayozidi kuwa mbaya.Suluhu ya kudumu ni kuvifungua vivuko vya kuingia Gaza ili bidhaa za misaada ya kibinadamu na ujenzi viweze kuingia.''alieleza.

Israel Palästina Palästinenser Siedlung Siedlungsbau Jerusalem Ramat Sholmo Ostjerusalem Flash-Galerie
Eneo la Jerusalem mashariki la Ramat Sholmo inakopanga Israel kuyajenga makazi mapya ya walowezi wa KiyahudiPicha: AP

Yote hayo yakiendelea ndege za kivita za Israel zimeripotiwa hii leo kulishambulia eneo la kusini mwa Gaza katika hujuma ya usiku kucha, baada ya wapiganaji wa Kipalestina kurusha kombora lililosababisha kifo cha mfanyakazi wa kigeni aliyekuwa Israel.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-RTRE/AFPE

Mhariri: Miraji Othman