1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa Brexit kuanza kabla ya uchaguzi wa Ujerumani

Yusra Buwayhid
2 Oktoba 2016

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, amesema anapanga kuwasilisha mswada wa kuifuta sheria iliyoiwezesha Uingereza kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, pia Uingereza itajiondoa kabla ya uchaguzi wa Ujerumani wa 2017.

https://p.dw.com/p/2Qo1E
London Demo gegen Brexit
Picha: picture-alliance/dpa/A. Rain

Akizungumza na gazeti la kila Jumapili la Uingereza "Sunday Times", Theresa May, ameahidi Uingereza litakuwa taifa huru na linalojitegemea ifikapo mwaka ujao, kwa kuibatilisha sheria iliyoifanya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Katika mahojiano hayo, May, ambae aliteuliwa baada ya Uingereza kupiga kura ya maoni ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya mwezi Juni, amesema ataanza mchakato wa kuiondoa nchi yake kutoka umoja huo kupitia ibara ya 50 ya Mkataba wa Lisbon, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Ujerumani Septemba mwaka ujao.

May ambae aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, amekuwa chini ya shinikizo kubwa la maafisa wa Umoja wa Ulaya, wawekezaji pamoja na wanachama wa chama chake cha kihafidhina kinachoongoza nchi, wanaomtaka atoe maelezo zaidi juu ya mpango wake wa kuiondoa rasmi Uingereza kwenye umoja huo.

Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano wa kila mwaka wa chama chake cha kihafidhina hapo jana, May anatarajia kuzima baadhi ya malalamiko kwa kuitengua sheria ya Jumuiya za Ulaya ya mwaka 1972, ambayo iliiruhusu Uingereza kujiunga na iliyokuwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya, ambayo baadae iligeuka kuwa Umoja wa Ulaya.

Njia rahisi ya Theresa May

Slowakei britische Peremierministerin Theresa May in Bratislava
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa MayPicha: Getty Images/AFP/S. Kubani

"Katika hotuba ijayo ya malkia wa Uingereza, tutawasilisha mswada mkubwa wa kuifuta sheria ya Jumuiya za Ulaya kwenye kitabu cha sheria za taifa," May ameliambi gazeti hilo. Ameongeza kuwa mshwada huo utawasilishwa mwezi Aprili au Mei.

"Hii ni hatua ya kwanza katika kuhakikisha kwamba Uingereza inarudi kuwa taifa huru na linalojitegemea. Ni hatua itakayorejesha nguvu na mamlaka katika taasisi zilizochaguliwa ndani ya taifa letu. Inaamanisha kwamba mamlaka ya Umoja wa Ulaya kwa Uingereza yatakuwa yamefikia kikomo," amesema May.

May amesema chini ya mipango yake hiyo, sheria ya Jumuiya za Ulaya ya mwaka 1972 itafutwa kabla ya Uingereza kuondoka rasmi katika umoja huo. Lakini kubatilishwa kwa sheria hiyo, kutatekelezwa rasmi kesheria  baada tu ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Kisha Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya (ECJ), haitakuwa tena na uwezo wa kutoa hukumu za kisheria dhidi ya Uingereza.

Mahakama ya ECJ ililaumiwa sana na wengi waliokuwa wakiunga mkono kampeni ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya kabla ya kupigwa kura ya maoni mwezi Juni, huku maafisa wa kambi iliyokuwa ikigombania kujiondoa katika umoja huo wakidai kuwa Uingereza ilishidwa kesi nyingi zilizohukumiwa na mahkama hiyo, katika kile walichokitaja kuwa "dhuluma."

Kiongozi wa Uingereza anatarajiwa kutumia Ibara ya 50, ili kuanza mchakato rasmi wa kuiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mapema mwaka ujao, hatua ambayo inaweza kuchukua hadi miaka miwili ya majadiliano, lakini ameweka wazi kuwa hataki kuelezea mipango yake kwa kina kabla ya mazungumzo hayo kuanza.

Großbritannien Kabinett David Davis Brexit-Minister
Waziri wa kusimamia mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, David DavisPicha: picture-alliance/empics/G. Fuller

May, ambaye aliteuliwa baada ya mtangulizi wake, David Cameron, kujiuzulu kufuatia kura ya maoni, pia amesema hakutakuwa na uchaguzi wa mapema wa bunge, akisema utalisababisha taifa hilo kile alichokiita "kuyumba" - jambo ambalo limekuwa likiwapa wasiwasi wawekezaji tangu wakati wa kura ya maoni.

Katika taarifa nyingine, waziri wake David Davis wenye wadhifa muhimu wa kusimamia mchakato wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (Brexit) amesema kwamba sheria ya Umoja wa Ulaya itabadilishwa na kuwa sheria ya Uingereza siku ambayo Uingereza itajitoa rasmi kwenye umoja huo. Sheria ambazo zilikuwa hazina ulazima hatimaye zitafutwa na bunge la nchi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afpr

Mhariri: Sudi Mnette