1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato waanza kutafuta kiongozi wa mpito Burkina Faso

6 Novemba 2014

Wanadiplomasia wanaowawekea shinikizo viongozi wa jeshi la Burkina Faso kukabidhi madaraka kwa raia, wameanza mchakato wa kumtafuta mtu atakayeongoza serikali ya mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.

https://p.dw.com/p/1DiBN
Mkutano wa wadau katika mchakato wa kutafuta serikali ya mpito ya Burkina Faso
Mkutano wa wadau katika mchakato wa kutafuta serikali ya mpito ya Burkina FasoPicha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Mazungumzo hayo ya jana yalisimamiwa na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, John Dramani Mahama wa Ghana na Macky Sall wa Senegal, yakiwashirikisha maafisa wa jeshi, viongozi wa vyama vya kisiasa na wawakilishi wa asasi za kiraia.

Ingawa washiriki waliafikiana juu ya kuwepo kwa utawala wa mpito kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambao utaongozwa na raia, hakukuwapo makubaliano juu ya kiongozi wa kipindi hicho. Rais wa Ghana John Dramani Mahama aliwaachia jukumu hilo wahusika nchini Burkina Faso.

''Na mtaendelea hadi pale mtakapompata mtu kutoka nchi hii, mwenye haiba, heshima, uaminifu na uzalendo ambaye ataweza kuiongoza Burkina Faso hadi mwakani, kwenye uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika. Hilo ndilo jukumu tunalowaachia kutekeleza.'' Alisema rais Mahama.

Rai ya kuepuka vikwazo

Rais Mahama alisema anaamini mchakato wa kumpata kiongozi huyo hautachukuwa wiki kadhaa, na kueleza matumaini yake kwamba haitakuwa lazima kwa jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo Burkina Faso. Umoja wa Afrika uliwapa wanajeshi wa Burkina Faso muda wa wiki mbili kukabidhi madaraka kwa raia, la sivyo wakabiliwe na vikwazo vya kiuchumi.

Rais wa Ghana John Dramani Mahama akitoa rai katika mkutano huo
Rais wa Ghana John Dramani Mahama akitoa rai katika mkutano huoPicha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon aliunga mkono juhudi za marais hao kutafuta suluhisho la amani katika mzozo huo wa Burkina Faso. Msemaji wake Stephen Dujarric amesema Umoja wa Mataifa unashirikiana na Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, kutafuta suluhisho la kudumu linalowahusisha wadau wote nchini humo.

Hali kadhalika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema pia linaunga mkono mchakato huo, na kuwataka wanajeshi kukabidhi madaraka na kuheshimu katiba ya nchi bila kuchelewa.

Ishara ya mvutano

Hata hivyo katika kile kilichochukuliwa kama ishara ya kupanda kwa joto la mvutano katika mkutano huo, wanasiasa wa upinzani pamoja na wanaharakati walitoka nje baada ya maafisa wa chama kilichokuwa madarakani kuingia katika mkutano huo.

Luteni Kanali Isaac Zida anayeshinikizwa kukabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraia
Luteni Kanali Isaac Zida anayeshinikizwa kukabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraiaPicha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Kiongozi wa asasi za kiraia Mathias Tankoano alisema hawawezi kukaa chumba kimoja na watu wanaotuhumiwa kusababisha vifo vya watu ambao hata bado hawajazikwa, na kuongeza kuwa maafisa hao wanapaswa kuhukumiwa kwa vifo hivyo, na kwa hila zao dhidi ya katiba ya nchi ambazo zililipeleka taifa katika ghasia.

Taarifa zilizotolewa baadaye zilisema Assimi Kouanda, kiongozi wa chama cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Blaise Compaore alikamatwa na polisi baada ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kuvuruga utulivu wa umma.

Burkina Faso iliingia katika mzozo wiki iliyopita baada ya kuibuka kwa maandamano yenye ghasia, kufuatia hatua ya aliyekuwa rais wake Blaise Compaore kujaribu kubadilisha katiba ili aweze kugombea mhula mwingine, kuendeleza utawala wake wa miaka 27. Baada ya kiongozi huyo kuikimbia nchi, aliyekuwa naibu kamanda wa kikosi cha kumlinda, Luteni Kanali Isaac Zida aliteuliwa na jeshi kuchukua madaraka ya kuiongoza nchi hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo