1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchinjaji mateka wa IS 'Jihadi John' ni raia wa Uingereza

27 Februari 2015

Mwanamgambo anayejulikana kwa jina la utani 'Jihadi John' wa kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la dola la kiislamu IS, ambaye amekuwa akionekana katika video akiwachinja mateka ametambuliwa kama Mohammed Emwazi

https://p.dw.com/p/1EiWe
Picha: Reuters//SITE Intel Group

Mohammed Emwazi ni raia wa Uingereza, mtaalamu wa masuala ya programu za kompyuta anayetokea familia inayojiweza iliyoko mjini London na alikuwa akifahamika na maafisa wa usalama nchini Uingereza hata kabla ya kuelekea Syria.

Mwanamgambo huyo ambaye huonekana katika video za kundi la IS akiwa amevalia nguo nyeusi na kuufunika uso wake, kushikilia kisu na kuzungumza kizungu anaaminika kuwa mchinjaji wa mateka wa kundi hilo wakiwemo raia wa Marekani, Uingereza na Syria.

'Jihadi John' kama anavyojulikana kwa jina la utani kutokana na lahaja yake ya kiingereza ana umri wa miaka 26 na alitumia video hizo kutoa vitisho kwa nchi za magharibi na viongozi wake wakiwemo Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kabla ya kuwatisha mateka ambao huwa wamevalishwa magwanda ya rangi ya chungwa.

Emwazi ni mzaliwa wa Kuwait

Emwazi amefichuliwa leo kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari vya Uingereza ambavyo vimeripoti alizaliwa Kuwait na alikwenda Uingereza na familia yake akiwa na umri wa miaka sita.

Mohammed Emwazi kwa jina jingine Jihadi John
Mohammed Emwazi kwa jina jingine Jihadi JohnPicha: Reuters//SITE Intel Group

Alihitimu na digrii ya masuala ya kompyuta kutoka chuo kikuu cha Westminister na shirika la ujasusi la Uingereza MI5 lilianza kufuatilia nyendo zake. Hayo ni kulingana na mkurugenzi wa shirika la utafiti la Cage linalowatetea watuhumiwa wanaozuiwa kwa mashitaka ya ugaidi Asim Qureshi.

Qureshi amesema shirika hilo la ujasusi lilijaribu mara kadhaa kumsajili Emwazi kujiunga nalo na baadaye kumzuia kusafiri nje ya Uingereza na hivyo kumlazimu kutoroka bila ya kuiarifu familia yake. Inaaminika mwanamgambo huyo alisafiri kuelekea Syria mwaka 2012.

Serikali ya Uingereza imekataa kuzungumzia ufichuzi huo kumhusu jihadi John na kusema uchunguzi bado unaendelea.

Mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza yametumia mbinu kadhaa za uchunguzi zikwemo za kutambua sauti na sura pamoja na kuwahoji mateka walioachiwa huru na IS kumtambua mwanamgambo huyo.

Shirika la Cage limedai Emwazi alihisi mfungwa kwa kuandamwa na maafisa wa kijasusi. Inadaiwa Emwazi alizuiwa nchini Tanzania mwezi Agosti mwaka 2009 alipokwenda kwa safari ya kitalii na marafiki zake wawili.

Huku hayo yakijiri, nchini Iraq wanamgambo wa IS wameharibu sanamu za kale za thamani kubwa ambayo ni sehemu ya turathi ya nchi hiyo katika mji wa Mosul.

IS yaharibu vito vya thamani Iraq

Uharibifu huo umeibua shutuma kali kutoka kwa wataalamu wa turathi na wanaaikolojia walioufananisha na ule uliofanywa na kundi la Taliban nchini Afghanistan mwaka 2001.

Wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu IS
Wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu ISPicha: picture-alliance/abaca/Yaghobzadeh Rafael

Shirika la umoja wa Mataifa la tamaduni na turathi limetaka kuitishwa mkutano wa dharura wa baraza la usalama la umoja huo kujadili uharibifu huo ambao limeutaja sehemu muhimu ya usalama wa Iraq.

Hayo yanakuja huku hofu ikitanda nchini Iraq na Syria baada ya kuripotiwa kuwa wanamgambo hao wamewateka nyara zaidi ya wakristo 220 katika kipindi cha siku tatu zilizopita.

Marekani na washirika wake zimefanya mashambulizi kumi na nne katika nchi hizo mbili tangu Jumatano asubuhi dhidi ya ngome za IS.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri:Josephat Charo