1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cambodia yaikubali meli iliyokataliwa kwa hofu ya COVID-19

Amina Mjahid
14 Februari 2020

Cambodia imeiruhusu meli moja ya kifahari kutia nanga kwenye bandari yake baada ya kukataliwa na mataifa mengine matano kwa hofu ya ugonjwa hatari wa COVID-19 unaotokana na virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3Xlz0
Kambodscha Kreuzfahrtschiff Westerdam eingetroffen
Picha: Reuters/Str

Mamia ya abiria walishangilia walipowasili na kushuka katika meli hiyo nchini Cambodia, ambapo walikaribishwa na kiongozi wa nchi hiyo, Hun Sen, aliyewapa maua. Waziri mkuu huyo aliamua kuiruhusu meli hiyo ya Westerdam kutia nanga katika bandari ya Sihanoukville hapo jana baada ya Thailand , Japan, Taiwan, Ufilipino na Guam kukataa kuiruhusu katika nchi hizo.

Wakati abiria wa kwanza aliposhuka kutoka meli hiyo, Hun Sen alisema kuwa ijapokuwa Cambodia ni nchi maskini, wakati wote imeungana na jamii ya kimataifa kutatua matatizo yanayoikumba dunia na eneo lao.

Meli hiyo ya Westerdam ilizuiliwa kutia nanga kwengineko ijapokuwa kampuni inayoimiliki ya Holland America Line inasema hakuna visa vya ugonjwa wa COVID-19 vilivyothibitishwa miongoni mwa abiria wake 1,455 na wafanyikazi 802.