1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli ya Marekani yawasili bandari ya Mombasa

Charo Josephat/RTRE12 Aprili 2009

Maharamia waonya dhidi ya kumuokoa nahodha

https://p.dw.com/p/HV8f
Meli ya Marekani "Maersk Alabama" ikijiandaa kutia nanga katika bandari ya Mombasa nchini KenyaPicha: AP

Meli ya Marekani "Maersk Alabama", iliyotekwa nyara kwa muda mfupi na maharamia wa kisomali, imewasili salama katika bandari ya Mombasa nchini Kenya. Meli hiyo ilikuwa imebeba msaada wa kimataifa wakati maharamia wa kisomali walipojaribu kuiteka wiki hii.

Afisa wa Marekani amesema meli hiyo ni eneo la uhalifu na kwa hiyo watu hawaruhusiwi kuingia. Maafisa wa idara ya upeplezi ya Marekani, FBI, watafanya uchunguzi kwamba kabla watu kuruhusiwa kuzungumza na wafanyakazi wa meli ya Maersk Alabama. Afisa huyo pia amesema wanafahamu chakula wanachohitaji wafanyakazi hao na kwamba watawapelekea wakati wakiendelea kubakia ndani ya meli hiyo mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Crew der Maersk Alabama im Hafen von Mombasa
Wafanyakazi wa meli ya Marekani "Maersk Alabama" baada ya kutia nanga mjini MombasaPicha: AP

Maharamia wa kisomali wanaomzuilia nahodha wa wa meli hiyo, Richard Phillips, wameonya kwamba matumizi ya nguvu kujaribu kumuokoa nahodha huyo huenda yakasababisha msiba. Nahodha huyo anazuiliwa kwenye boti ya uokozi ambayo bado iko katika eneo la kimataifa katika bahari ya Hindi. Jeshi la maji la Marekani lina manuwari tatu za kivita karibu na eneo hilo.

Maafisa wa jeshi la Marekani wamesema maharamia wameifyatulia risasi ndege ya Marekani iliyokuwa ikiikaribia boti hiyo, lakini hakuna aliyejeruhiwa. Boti hiyo inakaribia pwani ya Somalia na maafisa wana wasiwai maharamia huenda wakakimbia na mateka huyo watakapofika nchi kavu.

Nahodha Phillips ni mmoja wa mateka wa rehani 270 wanaozuiliwa na maharamia wa kisomali wanaoendesha uharamia katika ghuba ya Aden na katika bahari ya Hindi.

Wakati huo huo, inaripotiwa kwamba maharamia wa kisomali wameiteka nyara boti ya kuvuta meli kubwa inayomilikiwa na Marekani katika ghuba ya Aden. Boti hiyo, yenye bendera ya Italia, ina wafanyakazi 16.