1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MELI YAZAMA ZANZIBAR,43 WAFA

Abdu Said Mtullya10 Septemba 2011

Watu 43 wamethibitika kuwa wamekufa baada ya meli kuzama kisiwani Zanzibar

https://p.dw.com/p/12WZA
Rais wa Zanzibar Dr.Ali Mohamed SheinPicha: DW

Meli iliyokuwa na abiria zaidi ya mia tano ikiwa njiani kutoka Zanzibar kuelekea kisiwani Pemba nchini Tanzania imezama na watu wasiopungua 43 wamekufa.

Waziri wa nchi anaeshughulikia hali za dharura kisiwani Zanzibar, Mohammed Aboud amethibitisha kwamba maiti za watu 43 zimepatikana lakini ameeleza kuwa watu wengine wameokolewa na kati ya hao 40 wamejeruhiwa vibaya.Waziri Aboud amesema kuwa Zanzibar imeomba msaada kutoka Dar- Es -Salaam.

Hapo awali Kamishna wa Polisi ya Zanzibar Mussa Ali Mussa aliliambia shirika la habari, Reuters kwamba abiria 260 ikiwa pamoja na watoto 20 waliweza kuokolewa. Kamishna huyo ameeleza kuwa waokoaji wanaotumia mashua za uvuvi wanasaidia katika juhudi za kuwaokoa abiria zaidi.

Sababu ya kutokea ajali hiyo bado haijajulikana lakini baadhi ya abiria walionusurika wamelalamika kwamba meli hiyo ilijaa kupita kiasi. Kwa mujibu wa taarifa chombo hicho kilikuwa na shehena nzito ya mchele na bidhaa nyingine.

Meli ya "MV Spice Islander" iliyokuwa inasafiri kutoka kisiwani Unguja kwenda Pemba iliondoka Ugunja saa tatu asubuhi na ilizama muda wa saa nne baadae. Kwa mujibu wa taarifa watu wapatao 300 bado hawajulikani walipo.

Maafisa wa serikali wamesema kwamba watu karibu 600 wanasemekana kuwa walikuwamo katika meli hiyo, ikiwa pamoja na familia za watu waliokuwa wanarejea nyumbani baada ya kusherehekea mwisho wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

Juhudi za kuwaokoa watu zaidi zinaendelea lakini pana ukosefu wa vitendea kazi.

Mnamo mwaka 2009 meli nyingine ilizama nchini Tanzania ambapo watu 6 walikufa na pia pana habari kwamba mara kwa mara pezuka myoto katika meli za mizigo.