1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanzo mpya kwa Volkswagen

24 Septemba 2015

Meneja Mkuu wa kampuni ya magari ya Ujerumani,Volkswagen,Martin Winterkorn amejiuzulu baada ya kushinikizwa kufanya hivyo kutokana na kashfa ya udanganyifu

https://p.dw.com/p/1GcOL
Aliekuwa Meneja Mkuu wa kampuni ya Volkswagen Martin Winterkorn
Aliekuwa Meneja Mkuu wa kampuni ya Volkswagen Martin WinterkornPicha: Getty Images/S. Gallup

Bwana Winterkorn hakuweza tena kuhimili shinikizo. Mpaka Jumanne iliyopita Winterkorn bado alikuwa anajaribu kukitetea kiti chake. Alitaka kuchukua hatua ili kujaribu kuunga tena wajihi wa kampuni ya Volkswagen.Alitaka kuweka kila kitu bayana juu ya udanganyifu uliofanywa na kampuni hiyo wa kuweka kifaa katika magari kilichoweza kuficha vipimo sahihi juu ya kuchafuka kwa mazingira.

Lakini jana jioni enzi ya Martin Winterkorn ilimalizika. Na kwa hakika hiyo ni hatua nzuri.Kuondoka kwake maana yake ni kujaribu kuirejesha sifa nzuri ya kampuni ya Volkswagen na ya sekta ya viwanda vya magari -sifa ya Ujerumani duniani kote.

Kampuni ya Volkswagen inahitaji mwanzo mpya.

Symbolbild - VW Deutschland Flagge
Picha: Getty Images/S. Gallup

Martin Winterkorn alikuwa meneja wa itikeli za kizamani.Alikuwa kama kiongozi wa ukoo badala ya kuwa mwenyekiti wa kampuni kubwa ya kimataifa. Mfumo huo ulishapitwa na wakati.

Winterkorn alipaswa kuachia ngazi kwa sababu hakuweza tena kuidhibiti kampuni yake.Hata hivyo Winterkorn ndiye alieiongoza kampuni ya Volkswagen mpaka ikafikia upeo wa juu kabisa duniani. Lakini kama jinsi ilivyo katika maisha, mafanikio haraka sana hufunikwa na migogoro.

Hadi hivi karibuni tu Winterkorn alihesabika kuwa meneja bora kabisa. Lakini sasa heshima hiyo imetoweka.

Bodi ya uongozi ya kampuni ya Volkswagen, iliyokutana hapo jana, haikuwa na njia nyingine, licha ile ya kumwambia bwana Winterkorn asante na kwaheri. Winterkorn hakutaka kuondoka kwa hiari yake. Na alikuwamo mbioni kuurefusha mkataba wake kwa miaka miwili mingine.Lakini ni wazi kwamba hilo lisingeliwezekana kutokana na utata wa kisheria baada ya kutokea kashfa.

Msimamo ulikuwa mmoja na thabiti miongoni mwa wajumbe wa bodi ya uongozi. Waajiriwa na wawakilishi wao walikuwa na wasi wasi juu ya wafanyakazi 600,000 wa kampuni ya Volkswagen walioko duniani kote. Na wenye hisa walikuwa na wasi wasi juu ya fedha zao na juu ya sifa ya kampuni.

Bila shaka jana ilikuwa siku ya mkosi mkubwa kwa bwana Winterkorn aliezoea kufanikiwa tu. Amefikia mwisho wa safari yake ndefu kazini.Lakini ni mwisho uliogubikwa na vurumai. Bwana Martin Winterkorn angeliweza kuyaepuka hayo laiti angelizisoma alama za nyakati na kumwachia mtu mwengine aukimbize mwenge.

Mwandishi:Neufeld Thomas

Mfasiri:Mtullya abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga