1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aisifu Ugiriki kwa hatua za kubana matumizi

Sylvia Mwehozi
11 Januari 2019

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemsifu waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na kuonyesha mshikamano kwa nchi hiyo juu ya hatua za kubana matumizi, wakati alipotembelea mjini Athens siku ya Alhamis.

https://p.dw.com/p/3BMgg
Griechenland | Merkel zu Besuch
Picha: picture-alliance/dpa/A. Tzortzinis

Ziara ya  Merkel nchini Ugiriki imekuwa tofauti na ziara yake iliyopita ya mwaka 2014, ambapo alikabiiwa na maandamano ya hasira juu ya hatua za kubana matumizi.

Merkel amemsifu Tsipras kwa "hatua za maamuzi" juu ya mgogoro wa kuzozania jina na Macedonia. Nchi hiyo jirani ya Macedonia ambayo ilikuwa sehemu ya zamani ya Yugoslavia ina jina sawa na jimbo linalopatikana kaskazini mwa Ugiriki.

Tsipras na waziri mkuu mwenzake wa Macedonia Zoran Zaev wamekubaliana kubadili jina hilo na sasa itaitwa Jamhuri ya Macedonia ya Kaskazini. 

Griechendland, Athen: Proteste gegen den Staatsbesuch von Angela Merkel
Waandamanaji mjini Athens wakipinga ziara ya MerkelPicha: Reuters/A. Konstantinidis

"Makubaliano ya kubadili jina na Macedonia ya kaskazini, ni kwa ajili yetu sote. Nikizungumza kwa niaba ya Ujerumani, inaleta uwazi na itairuhusu Jamhuri ya Macedonia ya Kaskazini kujiunga na Jumuiya ya NATO pamoja na Umoja wa Ulaya. Hii sio tu italeta manufaa kwa Macedonia ya Kaksazini lakini pia itasaidia Ugiriki, kwasababu inaeleza jinsi mahusiano yanavyostawi na kuturuhusu sote kuunda mkakati wa umoja. Hiyo ndiyo sababu tunatoa fursa za Ulaya kwa nchi za Magharibi mwa Balkan ili kukuza maendeleo, " alisema Merkel.

Lakini wabunge wa Skopje ambao ni mji mkuu wa Macedonia bado watapiga kura kupitia hatua ambayo inajumuisha marekebisho manne ya kisheria na inahitaji kuungwa mkono kwa theluthi mbili kwenye bunge. Waziri Mkuu Tsipras ameyaelezea kwa "makubaliano ya mfano" yatakayoleta utulivu na ukuaji katika ukanda mzima.

Merkel aliitembelea Macedonia kabla ya kura ya maoni ya mwaka jana katika juhudi za kuonyesha mshikamano. Hata hivyo suala hilo bado lina mgawanyiko nchini Ugiriki ambako chama kimoja katika muungano tawala wa Tsipras kinapinga na kutishia wingi wake bungeni.

Griechenland, Athen: Staatsbesuch Angela Merkel und Prokopis Pavlopoulos
Kansela Merkel na rais wa Ugiriki Prokopis Pavlopoulos Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Rais wa Ugiriki Prokopis Pavlopoulos amemweleza Merkel alipokutana naye leo kwa mazungumzo kwamba Ugiriki ina misingi yote ya kutekeleza madai ya kisheria kwa mabilioni ya euro katika malipo ya utawala wa kinazi wakati wa vita ya pili ya dunia. Merkel amesema Ujerumani inawajibika kikamilifu kwa uhalifu uliofanywa na Wanazi nchini Ugiriki.

Pia suala lingine lililogusiwa ni pamoja na Ugiriki kutekeleza makubaliano ya wakimbizi kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ambapo Merkel amesisitiza wataendelea kushirikiana na Ugiriki kuboresha hali hiyo. Maelfu ya watu bado wanaendelea kuishi katika mazingira hafifu katika makambi ya wakimbizi kwenye visiwa vya Ugiriki vya Aagean, wakisubiri maombi yao ya hifadhi yashughulikiwe kuzingatia makubaliano hayo yaliyolenga kuzuia wimbi la wakimbizi na wahamiaji mwaka 2016. Watu karibu 200 walifanya maandamano katikati mwa Athens jana ya kumpinga Merkel.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/DPA

Mhariri: Yusuf Saumu