1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aitembelea Jamhuri ya Czech

3 Aprili 2012

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani yuko ziarani Jamhuri ya Czech ambako atakutana na waziri mkuu wa nchi hiyo Petr Necas pamoja na rais Vaclav Klaus.

https://p.dw.com/p/14WvG
Angela Merkel na Petr Necas mjini Prague
Angela Merkel na Petr Necas mjini PraguePicha: Reuters

Katika ziara yake ya siku moja mjini Prague, Kansela Angela Merkel atakutana na waziri mkuu wa Jamhuri ya Czech kuzungumzia mambo mbali mbali ikiwemo uhusiano baina ya Czech na Ujerumani. Mkataba wa Umoja wa Ulaya wa kudhibiti bajeti utajadiliwa pia. Katika hotuba aliyoitoa katika mtandao wa internet Jumamosi iliyopita, Kansela Merkel alisema kwamba anathamini sana uhusiano baina ya nchi yake na Jamhuri ya Czech. Alisema japo nchi hizi mbili wakati mwingine zilikuwa na mtazamo tofauti juu ya masuala kama vile matumizi ya nguvu ya nyuklia, daima zimekuwa zikifanya juhudi kupiga hatua za kimaendeleo.

Merkel alisisitiza kwamba uamuzi wa serikali ya Czech kutouunga mkono mkataba wa Umoja wa Ulaya wa kudhibiti bajeti si sababu ya kuzozana. Kwa maoni yake, nchi zinazoitumia sarafu ya Euro ndizo zinazopaswa kusaini mkataba wa kudhibiti bajeti. Na kwa kuwa Jamhuri ya Czech haiitumii sarafu hiyo, hailazimiki kusaini mkataba huo.

Waziri mkuu Petr Necas katika mkutano wa Umoja wa Ulaya
Waziri mkuu Petr Necas katika mkutano wa Umoja wa UlayaPicha: dapd

Czech huenda ikasaini mkataba wa kudhibiti bajeti

Heinz-Peter Haustein, ambaye ni mwanasiasa wa chama cha kiliberali cha FDP na mtaalamu wa masuala yanayoihusu Jamhuri ya Czech, ameliambia shirika la habari la hapa Ujerumani la dpa kwamba upo uwezekano wa Czech kusaini mkataba wa kudhibiti bajeti. Haustein alikumbusha kwamba maseneta wa Czech wiki iliyopita walikutana na mwenyekiti wa kamati inayoshughulikia masuala ya Ulaya katika Bunge la Czech, Ludek Sefzig. Katika mkutano huo, Sefzig alieleza kwamba anaona uwezekano wa nchi yake kusaini mkataba wa kudhibiti bajeti iwapo masuali yaliyoko sasa yakipatiwa ufumbuzi. Czech na Uingereza ni nchi pekee za Umoja wa Ulaya ambazo bado hazijasaini mkataba wa kudhibiti bajeti.

Mbali na kuzungumzia masuala ya siasa za ndani na nje, Merkel atazungumza na wenyeji wake juu ya sera za mazingira na nishati. Ujerumani ina wasiwasi mkubwa juu ya hali ya usalama ya kinu cha nyuklia cha Czech kiitwacho Temelin na kilichopo umbali wa kilometa 50 kutoka katika mpaka wa Czech na Ujerumani. Tangu kujengwa kwake mwaka 2002, kinu hicho kimekuwa kikiharibika mara kwa mara.

Kinu cha nyuklia cha Temelin
Kinu cha nyuklia cha TemelinPicha: AP

Leo mchana Angela Merkel atakutana na wanafunzi wa chuo kikuu cha Karls kilichopo mji mkuu Prague. Merkel atazungumza na wanafunzi hao kuhusu namna ya kuujenga mustakabali wa bara la Ulaya.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/dapd
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman