1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akataa kuweka kikomo cha wakimbizi

Yusra Buwayhid
17 Julai 2017

Kansela Angela Merkel ameweka wazi katika mahojiano, msimamo wake wa kuendelea kuiongoza Ujerumani kwa miaka mingine minne pamoja na kukataa pendekezo la kuweka kikomo cha idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini kila mwaka.

https://p.dw.com/p/2gduE
ARD-Sommerinterview mit Angela Merkel
Picha: Picture alliance/dpa/M. Gambarini

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anatarajia kuendelea kuiongoza Ujerumani katika miaka minne ijayo akiwa katika mahojiano yaliyorushwa jana katika televisheni, wakati kampeni za uchaguzi wa mwezi Septemba zikiwa zimeanza. Merkel ameyasema hayo katika mahojiano ya televisheni na kituo cha ARD hapo jana.

"Nilipotangaza kwamba nitagombea tena, niliweka wazi kuwa nitaendesha nchi kwa miaka minne .. Bila shaka sote tuna udhibiti mdogo juu ya maisha yetu, lakini nina nia ya kufanya kile nilichowaambia watu. Hiyo ni sehemu ya uaminifu," amesema Angela Merkel.

Katika mahojiano yake na ARD, kansela huyo aliyepo madarakani amezungumzia pia masuala ya wakimbizi na uwekezaji, pamoja na uhusuano wa Ujerumani na Uturuki na jumuiya kujihami ya NATO.

Kiongozi huyo wa Ujerumani hakuwa na hofu ya kutetea misimamo yake anayoiamini. Licha ya mvutano na chama ndugu cha kihafidhina cha Christian Social Union (CSU), Merkel, anayeongoza chama cha Christian Democratic Union (CDU) amekataa wito wa kupunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini Ujerumani.

Wakimbizi hawatowekewa kikomo

"Nina msimamo wa wazi kuhusu pendekezo la kuweka kikomo cha idadi ya wakimbizi wanaoingizwa nchini, na ninasema 'sitakubali'. Nakubaliana na mtazamo kwamba tunahitaji kupunguza uhamiaji wa moja kwa moja na tunahitaji kupambana na sababu zinazosababisha uhamiaji, na nadhani kwa njia hii tunaweza kufikia malengo yetu bila kuweka kikomo, " amesema Angela Merkel.

Msimamo wake huo unamfanya agongane na kiongozi wa CSU, Horst Seehofer, ambaye ametishia kutokubali kuunda serikali ya muungano, bila ya kikomo cha idadi ya wahamiaji wataoingia Ujerumani kila mwaka.

Berlin SPD-Kanzlerkandidat Schulz präsentiert Zukunftsplan
Kiongozi wa chama cha Social Democratic, SPD, Martin SchulzPicha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Wakati alikubaliana na mpinzani wake wa chama cha Social Democratic, SPD, cha siasa za mrengo wa kushoto wa wastani, Martin Schulz, juu ya haja ya uwekezaji katika masuala ya kidijitali, Merkel amedai kwamba tatizo kubwa si ukosefu wa fedha bali ni mchakato wa mipango ya muda mrefu.

Akiizungumzia Uturuki, Merkel amesema wabunge wa Ujerumani waruhusiwe kuwatembelea wanajeshi wao katika kambi ya jeshi la anga ya Shirika la kujihami NATO iliyopo Konya, Uturuki, na kwamba mazungumzo zaidi yanahitajika kutatua mzozo kati yao.

Na alipoulizwa juu ya machafuko yaliyotokea mapema mwezu huu wakati wa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi na yanayoinukia haraka kiuchumi duniani, G20, katika mji wa bandari wa Hamburg, Merkel amesema maandamano yaliyotokea hayakubaliki kabisa lakini bado ulikuwa ni uamuzi mzuri kuwaalika viongozi wa kundi la G20 mjini Hamburg.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpae

Mhariri: Josephat Charo