1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akosolewa ndani ya chama chake cha CDU

Bruce Amani
9 Februari 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanachama wa chama chake cha kihafidhina cha Christian Democratic Union – CDU baada ya kulazimika kuziachia nyadhifa kuu za uwaziri

https://p.dw.com/p/2sOKD
Koalitionsverhandlungen von Union und SPD
Picha: AFP/Getty Images

Chama cha SPD kilinyakua wizara muhimu za fedha, mambo ya nje na wizara yenye bajeti kubwa ya kazi na masuala ya kijamii kama sehemu ya makubaliano yaliyofikia Jumatano.

Hisia za kutoridhishwa ndani ya chama cha CDU zinaonekana kuugubika mkutano mkuu wa chama mnamo Februari 26, ambao umeitishwa kwa ajili ya kupiga kura kuhusu makubaliano hayo ya muungano ambayo Merkel aliyafikia na SPD baada ya majadiliano yaliodumu kwa zaidi ya wiki tatu.

Koalitionsverhandlungen von Union und SPD  Martin Schulz
Martin Schulz, kiongozi wa SPDPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Matokeo yake ni kuwa mkutano huo wa CDU huenda ukageuka kuwa mtihani mkubwa wa mamlaka ya kisiasa ya Merkel baada ya zaidi ya miaka 12 akiwa Kansela.

Tawi lenye nguvu kabisa la wafanyabiashara wa CDU katika jimbo la kusini magharibi la Baden Wuerttemberg limesema limekasirishwa na mpango wa kutoa nyadhifa tatu muhimu kwa SPD, ambacho kilipata tu asilimia 20.5 ya kura katika uchaguzi wa Septemba. Lakini Horst Seehorfer, kiongozi wa Christian Social Union – CSU, washirika wa Bavaria wa chama cha Merkel CDU, amewaambia wanahabri kuwa SPD kilisisitiza kuwa kilitaka wizara hizo tatu, la sivyo hawangejiunga na serikali.

Makubaliano hayo yalioko kwenye kurasa zaidi ya 170 yanakabiliwa na kura isiyotabirika ya Zaidi ya wanachama 460,000 wa SPD. Karibu asilimia 76 ya wanachama wa SPD waliunga mkono kuunda muungano na kundi la vyama vya CDU/CSU baada ya uchaguzi wa 2013.

Wakati huu hata hivyo, sehemu kuwa ya chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto inapinga kujiunga kwa miaka mingine minne kama mshirika mdogo wa muungano unaoongozwa na Merkel baada ya kupata matokeo mabaya Septemba.

Deutschland Koalitionsverhandlungen von Union und SPD | Außenminister Sigmar Gabriel
Sigmar Gabriel amkosoa Schulz kwa kuvunja ahadiPicha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Matokeo ya kura ya SPD yatatangazwa Machi nne. Kama wataunga mkono serikali mpya ya muungano hatua hiyo itamaliza miezi kadhaa ya sintofahamu ya kisiasa katika taifa hilo ambalo ni kubwa kiuchumi Ulaya. Kama chama hicho kitapinga, basi huenda uchaguzi mpya ukaitishwa, au kukawa na uwezekano wa kuunda serikali ya wachache ikiongozwa na CDU/CSU

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Kigeni anayeondoka Sigmar Gabriel amemtolea maneno makali Martin Schulz na chama cha Social Democratic - SPD ambacho alikiongoza kwa miaka nane, kuanzia 2009 hadi 2017. Katika mahojiano na magazeti ya chombo cha habari cha Funke, Gabriel amelalamika kuhusu ukosefu wa shukrani kutoka kwa uongozi mpya wa Schulz katika SPD kutokana na kazi yake akiwa Waziri wa mambo ya nje, kazi ambayo alisema, ilisifiwa na wengi. Kulikuwa na uvumi Schulz alikuwa amemhakikishia Gabriel kuwa angehifadhi wadhifa wake kama waziri wa mambo ya kigeni katika serikali mpya. Hata hivyo, siku ya Jumatano, Schulz alisema anataka kazi ya waziri wa mambo ya nje, hata ingawa alikuwa amesema baada ya uchaguzi wa Septemba kuwa hatohudumu katika baraza la mawaziri linaloongozwa na Kansela Angela Merkel.

Mwandishi. Bruce Amani/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga