1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Obama Washington

9 Februari 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anatazamiwa kutetea hoja yake ya kupinga kuipatia silaha Ukraine katika mzozo wake na waasi wakati atakapokutana na Rais Barack Obama wa Marekani mjini Washington.

https://p.dw.com/p/1EYcW
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Barack Obama wa Marekani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: picture-alliance/dpa

Ujumbe wa Merkel kwamba kupeleka silaha za mataifa magharibi kwa serikali ya Ukraine kunahatarisha kuupalilia mzozo huo yumkini ukatiliwa maanani wakati atakapokutana na Rais Barack Obama wa Marekani Jumatatu.(09.02.2015)

Lakini wakosoaji wa sera ya kigeni ya tahadhari ya Obama tayari wamekuwa wakidai serikali ya Marekani ichukuwe hatua madhubuti kuisaidia serikali ya Ukraine kupambana na waasi mashariki mwa nchi hiyo hata kama itaukuza mzozo huo na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Merkel ambaye pamoja na Rais Farncois Hollande wa Ufaransa wanatazamiwa kukutana na Rais Putin mjini Minsk hapo Jumatano wamekuwa wakishutumiwa na wabunge wa Marekani wanaopendelea sera ya kigeni ya mabavu katika bunge la Marekani lenye kudhibitiwa na chama cha Republikan ambao wanataka silaha za kujihami zitumwe kwa jeshi la Ukraine.

Mablanketi hayasaidii kupambana na vifaru

Seneta John McCain amekaririwa akisema katika Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba "Waukraine wamekuwa wakiuwawa na wao wamekuwa wakiwapelekea mablanketi ambayo hayasaidii kitu kukabiliana na vifaru vya Urusi."

Seneta John McCain wa Marekani.
Seneta John McCain wa Marekani.Picha: Reuters/M. Dalder

Lakini Merkel ametamka wazi msimamo wake wa kuipatia silaha serikali ya Ukraine kwa kusema kwamba "anafahamu mjadala huo lakini anaamini kutolewa kwa silaha zaidi hakutopelekea kupatikana kwa maendeleo inayoyahitaji Ukraine na kwamba anatilia shaka sana jambo hilo."

Merkel ambaye anazungumza lugha ya Kirusi na ambaye amekulia Ujerumani ya mashariki amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhisho la kidiplomasia ambapo amezungumza na Putin mara kadhaa katika kipindi cha mwaka mmoja na kukutana naye nchini Urusi, Australia na Italia katika miezi ya hivi karibuni.

Putin hathubutu kuwekewa muda wa mwisho

Serikali ya Urusi imeonya leo hii kwamba Putin hawezi kuzungumziwa katika lugha ya vitisho vya kumuwekea muda wa mwisho kutekeleza maagizo. Alipoulizwa juu ya tetesi za vyombo vya habari kwamba Merkel alimpa muda mwisho Putin katika mazungumzo ya kutayarisha mkutano wa kilele wa Minsk, msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov ameiambia radio ya Govorit Moskva kwamba "hakuna mtu aliyewahi katu kuzungumza na rais huyo kwa lugha ya kumpa muda wa mwisho na hawawezi kufanya hivyo hata kama wangelitaka iwe hivyo."

Rais Vladmir Putin wa Urusi.
Rais Vladmir Putin wa Urusi.Picha: Getty Images/AFP/A.Nikolsky

Obama inabidi aamuwe iwapo atume silaha kwa Ukraine,iweke vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi kwa matarajio ya kumlazimisha Putin akubali kufikia muafaka au aunge mkono kikamilifu juhudi mpya za kutafuta amani za Ujerumani na Ufaransa.

Maafisa wa serikali ya Marekani wanasema atatafakari maamuzi yake kwa uangalifu na hatofanya pupa katika kutowa uamuzi.

Tayari kiongozi huyo ana mapendekezo mezani mwake juu ya hasara na manufaa ya kuipatia Ukraine silaha kama zile za kupambana na vifaru,silaha ndogo ndogo na risasi.

Baadhi ya washauri wake wakuu akiwemo yule aliyemteuwa kuwa waziri mpya wa ulinzi Ashton Carter wanapendelea kusaidiwa kijeshi kwa Ukraine.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Yusuf Saumu