1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akutana na Putin mjini Sochi

Zainab Aziz
2 Mei 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mazungumzo na rais wa Urusi Vladimir Putin huku Merkel akiupa umuhimu zaidi uhusiano baina ya Ujerumani na Urusi akisema kuwa Urusi ni mshirika muhimu sana.

https://p.dw.com/p/2cExZ
Russland | Merkel trifft Putin
Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/S. Guneev

Hii ilikuwa ni ziara ya pili nchini Urusi ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel tangu nchi hiyo ilipolitwaa jimbo la Crimea lililo magharibi mwa Ukraine miaka mitatu iliyopita.  Kansela Merkel amefanya ziara yake katika mji wa Sochi. Miji ya Sochi na Crimea iko katika bahari nyeusi. Kansela Angela Merkel alimwambia rais Vladimir Putin kuwa Urusi ni mshirika muhimu pale walipokutana kwenye mji wa kusini wa mapumziko wa Sochi.  Viongozi hao walifanya mazungumzo yao katika makao ya rais Putin ya Bocharov Ruchei.

Kansela wa Ujerumani amesema amekuwa na mazungumzo yenye muelekeo mzuri na rais Putin ambayo yaligusia mambo mengi ikiwa ni pamoja na migogoro ya Syria na Ukraine.Kansela Merkel amesema walizungumzia pia kuhusu maswala ya haki za binadamu ambapo bibi Merkel aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alimuomba rais Putin atumie ushawishi wake kulinda haki za makundi ya watu wachache kama vile watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja huko Chechnya kutokana na ripoti kuwa watu hao wananyanyaswa na kuuwawa. 

Russland | Pressekonferenz Merkel Putin
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

Kansela Merkel amesema anataka kuendelea kutafuta suluhisho la mizozo ya dunia na kwamba Urusi ina jukumu kubwa pia. Kwa upande wake rais wa Urusi Vladimir Putin amesema amemwambia kansela wa Ujerumani kwamba Urusi inalaani mashambulio yoyote kwa kutumia silaha za sumu hivyo basi angetaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini aliyefanya mashambulio ya mwezi uliopita nchini Syria katika mji wa Khan Sheikhon. Putin amesema watakaopatikana na hatia ya kutenda mauaji hayo waadhibiwe. 

Putin amesema pia,  suluhisho nchini Syria litapatikana tu kwa njia ya amani chini ya Umoja wa Mataifa. Vile vile rais Putin amemshukuru kansela wa Ujerumani kwa kujadili pamoja naye juu ya mipango ya mkutano mkuu wa wanachama wa kundi la G20 unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani.

Wakati huo huo Putin amekanusha kuwa nchi yake ilihusika kivyovyote vile katika kuingilia matokeo ya uchaguzi wa rais ya mwaka uliopita nchini Marekani. Viongozi hao walipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wao walisema kuwa lawama hizo za kuingiliwa uchaguzi wa Marekani ni uzushi unaotumiwa kwenye siasa za ndani huko nchini Marekani.

Mwandishi: ZAinab Aziz/RTRE/APE

Mhariri:Iddi Ssessanga