1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aonya 2010 utakuwa mgumu kwa uchumi wa Ujerumani

1 Januari 2010

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ameonya kuwa msukosuko wa uchumi bado haujamalizika lakini kuna matumaini ya kuona siku za neema.

https://p.dw.com/p/LI5N
30.12.2009 DW-TV JOURNAL Angela Merkel 1
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Kansela Angela Merkel katika hotuba yake ya mwaka mpya kwa taifa amesema mwaka 2010 ni mwaka muhimu utakaoamua vipi Ujerumani itakavyojitoa kwenye msukosuko wa uchumi.

Merkel ameeleza waziwazi kuwa Wajerumani wasitaraji kuona mzozo wa uchumi ukimalizika haraka. Amesema, baadhi ya mambo katika mwaka mpya yatakuwa magumu kweli ,kabla ya kuanza kuwa bora. Hata hivyo, kuna sababu nzuri ya kuamini kwamba Ujerumani itadhibiti mzozo huo na uchumi wake utaibuka imara zaidi kuliko vile ulivyokuwa ulipotumbukia katika janga hilo.

Wakati huo huo Merkel amesema, licha ya uchumi dhaifu kusababisha matatizo kwa nchi zilizoendelea, hali hiyo isiyazuie mataifa hayo kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa baada ya kutofanikiwa kwa mkutano wa mazingira uliofanyika mwezi wa Desemba mjini Copenhagen.