1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel arejea tena katika uchaguzi jimboni Lower Saxony

Sekione Kitojo
15 Oktoba 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakabiliwa leo(15.10.2017)na mtihani katika uchaguzi wa jimbo, baada ya kushinda muhula wa nne kwa kupata ushindi mwembamba uliomlazimu kuingia mazungumzo magumu ya kuunda serikali.

https://p.dw.com/p/2lrDG
Landtagswahl Niedersachsen
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gentsch

Wiki tatu baada ya wapiga kura nchini Ujerumani kukika chama cha kansela  Merkel cha Christian Democratic Union matokeo yake mabaya kabisa katika muda wa miongo kadhaa, kiongozi huyo wa nchi yenye uchumi mkubwa kabisa katika Umoja  wa  Ulaya anakabiliwa  na  uchaguzi  mwingine , mara  hii  katika  jimbo  la Lower Saxony.

Deutschland Frankfurter Buchmesse 2017 Eröffnung Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/A. Dedert

Vituo vya  kupigia  kura  vilifunguliwa  majira  ya  saa mbili  asubuhi saa  za  Ulaya  ya  kati  kwa  ajili  ya  wapiga  kura  milioni  6.1 walioandikishwa  kupiga  kura  na vinatarajiwa  kufungwa saa  12 jioni wakati makadirio  ya  kwanza  yatakapotolewa katika televisheni  ya  umma.

Uchunguzi  wa  hivi  karibuni  wa  maoni  ya  wapiga  kura yanaonesha  kwamba  chama  cha  CDU kiko  nyuma  ya  chama cha  Social Democratic SPD  katika  jimbo hilo, jimbo  la  nne  kwa idadi  ya  watu  nchini  Ujerumani na  mahali  kilipo  kiwanda cha kutengenezea  magari  ya  Wolkswagen  kilichokumbwa  na kashfa.

"Ushindi  katika  jimbo  la  Lower Saxony  ni  muhimu kwa  Merkel kwasababu  utamuimarisha na  kuonesha  kwamba  chama  chake kinaweza  bado  kushinda  chaguzi  za  majimbo," amesema  Oskar Niedermayer  wa  chuo  huria  cha  mjini  Berlin.

Deutschland Landtagswahl Niedersachsen | Weil und Althusmann  | Plakate
Mabango ya uchaguzi wa jimbo la Lower Saxony nchini UjerumaniPicha: Getty Images/D. Hecker

Lakini  kushindwa "kutakuwa  ishara  mbaya  kwa ajili  ya majadiliano  ambayo  yanaanza  katikati  ya  wiki ijayo" ya  kuunda serikali  mpya  ya  mseto mjini  Berlin, gazeti  maarufu  nchini Ujerumani  la  Bild  limesema  leo  Jumapili(15.10.2017).

SPD yawania ushindi

Mpizani  wa Merkel , kiongozi  wa  chama  cha  SPD Martin Schulz , pia anawania kupata  ushindi  katika  uchaguzi  huo , baada  ya kipingo cha  kudhalilisha  katika  uchaguzi  wa  taifa.

Jimbo  la  Lower  Saxony limelazimika  kufanya  uchaguzi  wa mapema  baada  ya  muungano  uliokuwa  ukitawala  katika  jimbo hilo  wa  chama  cha  SPD  na  chama  cha  kijani  kuvunjika kilipopoteza  wingi  wake  mdogo kutokana  na  kujitoa kwa  mbunge mmoja  chamani.

Muungano  dhaifu  kama  huo  utakuwa  haswa  kile  Merkel anachotaka  kukiepuka  wakati  akifungua  mazungumzo  na washirika  watarajiwa  siku  ya  Jumatano.

Deutschland Landtagswahl Niedersachsen | Weil und Althusmann
Waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony Stephan Weil na mgombea wa CDU Bernd AlthusmannPicha: picture alliance/dpa/J. Stratenschulte

Lakini  baada  ya  miaka  12 madarakani  katika  nchi  hiyo  yenye uchumi  mkubwa  katika  Umoja  wa  Ulaya , sasa  anakabiliwa  na moja  kati  ya  changamoto  kubwa  kabisa: kuwabadilisha washirika wa kisiasa ambao  ni  wapinzani  kuwa  washirika  wenza.

Iwapo  atafanikiwa , Ujerumani  inaweza  kupata  serikali  yake  ya kwanza  ya  mseto  ya  kundi  la  kambi  yake  ya  kihafidhina, waliberali na wanaopendelea  biashara  chama  cha  Free Democrats , FDP  na  chama  cha  walinzi  wa  mazingira , cha  kijani iwapo  watashindwa  kufikia  makubaliano , Merkel atawajibika kuitisha  upya  uchaguzi.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri Lilian Mtono