1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ataka hatua kali za COVID-19 kuelekea Krismasi

Sylvia Mwehozi
9 Desemba 2020

Katika hotuba yake kwa bunge Jumatano, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa hatua kali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3mUE2
Deutschland Bundestag Generaldebatte zum Bundeshaushalt
Picha: Tobias Schwarz/AFP/Getty Images

Kansela Merkel ametoa wito wa vikwazo vikali katika shughuli za kila siku za umma kuelekea sikukuu za Krismasi. Ameonekana waziwazi kuunga mkono mapendekezo yaliyotolewa Jumanne na chuo cha taifa  cha sayansi, Leopoldina.

Katika mapendekezo yao wanataka shule zifungwe kuanzia Desemba 14, mapumziko ya Christmas kupanuliwa, kufungwa kwa biashara zote kasoro zile muhimu kuanzia Desemba 24 pamoja na kufanyia kazi kutokea nyumbani kwa kiasi kikubwa.

Merkel amesema anapinga kufunguliwa kwa hoteli ili familia ziweze kukutana wakati wa Christmas na mwaka mpya lakini anakubaliana na mapendekezo ya maduka yote kufungwa hadi Januari 10.

Kansela Merkel ametoa hotuba hiyo katika bunge la Ujerumani, Bundestag siku ya Jumatano, wakati wa mjadala wa bajeti ijayo ya serikali. Huu ndio utakuwa mjadala wa mwisho wa bajeti kwa Merkel, ambaye hatowania tena nafasi hiyo katika uchaguzi ujao, baada ya kukaa madarakani kwa miaka 15. 

Aidha amepuuzia ukosoaji wa namna serikali yake ilivyoshughulikia janga la virusi vya corona, akisema nchi hiyo ilikuwa ikipitia "hali ya kipekee". "Jambo muhimu katika kufanikisha mapambano dhidi ya virusi ni uwajibikaji wa tabia za kila mmoja wetu na utayari wa kushirikiana", Merkel amelieleza bunge.

Kulingana na takwimu za taasisi ya Ujerumani ya kupambana na magonjwa ya Robert Koch,idadi ya vifo vya kila siku iliongezeka Jumatano kufikia watu 590 na kufanya idadi jumla ya waliofariki tangu kuzuka kwa janga hilo kufikia 19,932 huku maambukizi yakipindukia milioni 1.2.

AfD yamshambulia Merkel

Baada ya hotuba yake, Merkel alikosolewa vikali na chama chenye mrengo mkali wa kulia, chama mbadala kwa Ujerumani AfD. Kiongozi mwenza wa AfD bungeni Alice Weidel ametoa wito wa kusitishwa "kwa hatua zisizofaa za vizuizi", na kulaumu kile alichokiita hatua za Merkel" zilizokosa malengo na zenye upotoshaji". „Anawafungia watu na kuharibu sekta nzima" alisema Weidel aliyedai hatua zitakuwa na maumivu zaidi badala ya kuleta manufaa.

Naye kiongozi wa chama kinachopendelea biashara cha Free Democrats FDP, Christian Lindner, amesema hatua za sasa za vizuizi ni "ishara tosha” kwamba hazifanya kazi na kwa kiasi kikubwa zimedhoofisha uhuru wa watu binafsi.

Ametoa wito wa ''mipango inayotabirika'' katika jitihada za serikali za kupambana na virusi hivyo na kuonya dhidi ya kile chama chake kinachokiona kama madhara yasiyostahili kwa biashara ya Ujerumani.

Pamoja na kwamba bunge lilikuwa lijadili bajeti, lakini kwa kiasi kikubwa lilitawaliwa na mapambano dhidi ya janga la virusi vya corona.

Merkel akiondoka atabakisha madeni

Kuhusu uchumi kiongozi wa AfD amesema urithi wa Merkel utakuwa na madeni na ukosefu wa ajira, akiongeza kuwa sekta ya magari imerudi nyuma chini ya siasa za Merkel za ulinzi wa mazingira. Wakati AfD ndio chama kikubwa cha upinzani katika bunge, chama cha kijani kinazidi kujisogeza mbele katika kura za hivi karibuni za maoni.

Merkel pia amekiri changamoto zinazoikabili Ujerumani katika ngazi ya Umoja wa Ulaya na kimataifa. Kansela huyo amesema ana matumaini kuwa Umoja wa Ulaya na Uingereza zitaweza kufikia makubaliano ya kibiashara kabla ya mwaka kumalizika.