1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atarajiwa kuhutubia bunge la Israel

Mwakideu, Alex18 Machi 2008

Wabunge watano wa Israel watishia kususia hotuba ya Merkel wakisema lugha ya kijerumani atakayohutubia nayo itazua hisia kali za wakati wa vita vya pili

https://p.dw.com/p/DQWg
Rais wa Israel Shimon Peres amkaribisha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika makao yake mjini JerusalemPicha: AP

Leo ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Israeli wabunge takriban watano wamesema watasusia hotuba inayotarajiwa kutolewa bungeni na Kansela huyo.


Wakati huo huo Kansela Merkel ametumia siku yake ya tatu nchini Isreali kukutana na Rais wa nchi hiyo Shimon Peres.


Kansela Merkel anatarajiwa kuhutubia bunge la Knesset leo jioni.


Mmoja wa wabunge walioahidi kususia hotuba yake ni Shelly Yachimovich mwanachama wa muungano wa chama cha Labour ambaye amesema hotuba hiyo itakayotolewa kwa lugha ya kijerumani itazua hisia kali kwa manusura wa Holocaust; mauaji yaliyotekelezwa na utawala wa Ujerumani kwa wayahudi wakati wa vita vya dunia vya pili.


Yachimovich ambaye ni binti ya mmoja wa manusura wa mauaji hayo amesema Ujerumani ni marafiki wa Israel lakini kuna umuhimu wa kutilia maanani hisia za watu hao.


Wabunge wawili kutoka chama cha upinzani chenye siasa kali cha Likud pamoja na wengine wawili kutoka chama cha kidini cha National Union wameunga mkono maneno ya Yachimovich. Watatu kati yao wamesema watasusia kabisa hotuba hiyo huku mmoja Arieh Eldad wa National Union akiahidi kuondoka bungeni mwanzoni mwa hotuba hiyo kama ishara ya kupinga utumizi wa lugha ya kijerumani katika bunge la Knesset.


Mwanachama mwenzake Yitzhal Levy ameambia vyombo vya habari kwamba licha ya Ujerumani kuonesha uhusiano mzuri na Israel Wayahudi wangali wanakumbuka yaliyojiri wakati wa vita vya dunia vya pili.


Hata hivyo mbunge mwengine mwenye miaka 73 ambaye ni nusura wa vita hivyo amesema mpango huo wa kususia hotuba ya Merkel ni njia ya kujitafutia umaarufu kwani yeye mwenyewe haoni ubaya wowote wa Kiongozi huyo wa Ujerumani kuhutubia kwa lugha anayoilewa zaidi.


Mwenzake kutoka chama cha Labour ambaye ni mwanaye nusura wa Holocaust Ophir Pines ameshutumu mpango huo akiutaja kama njia ya kuzua uhasama.


Kansela Angela Merkel ameanza ziara yake ya siku ya tatu nchini Israel kwa kukutana na Rais wa nchi hiyo Shimon Peres.


Anatarajiwa kufanya mazungumzo zaidi na wanasiasa wa Israel wakiwemo kiongozi wa upinzani Benjamin Netanyahu pamoja na waziri wa nchi za nje Tzipi Livni kabla ya kushiriki katika mjadala kuhusu jamii ya wakiristo nchini Israeli utakaoshirikisha viongozi wa makanisa nchini Ujerumani.


Hatimaye anatarajiwa kuhutubia bunge la Knesset leo jioni. Merkel ataingia katika vitabu vya historia kama mmoja wa viongozi wachache wa serikali kutoka nje waliohutubia bunge la Israel.


Vingozi ambao wamewahi kulihutubia ni marais wawili wa Ujerumani na Rais wa zamani wa Misri Anwar Sadat mwaka wa 1977.


Israel na Ujerumani zimeongeza zaidi uhusiano wao kwa kutia sahihi makubaliano ya kushirikiana katika maswala ya kijeshi, utamaduni, siasa na uchumi.


Leo imekuwa siku ya kwanza kabisa kwa Israel kuandaa mkutano na nchi ya nje unaoshirikisha wabunge 17 kutoka pande zote mbili wakiwemo Merkel na waziri mkuu wa nchi hiyo Ehud Olmert.