1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atembelea kituo cha ujumbe wa Umoja wa Ulaya Niger

Sekione Kitojo
3 Mei 2019

Kansela wa Ujerumani Angela  Merkel ametembelea ujumbe wa kutoa mafunzo wa Umoja  wa Ulaya kwa ajili ya majeshi ya usalama katika mji mkuu wa Niger-Niamey mwishoni mwa ziara yake ya siku tatu katika Afrika magharibi.

https://p.dw.com/p/3Htmy
Niger Kanzlerin Merkel auf Afrikareise | Merkel und Präsident Issoufou
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Maafisa  wa ujumbe  huo  wa  kujenga  uwezo  nchini  Niger EUCAP Sahel , walizungumza na  kansela  kuhusu  uhamiaji, ugaidi, uhalifu  wa kupangilia, ulinzi wa kutumia  magari  katika  mpaka na usafirishaji wa madawa  ya  kulevywa. 

Kanzlerin Merkel in Afrika
Kansela Angela Merkel akizungumza na wanajeshi wa Ujerumani nchini NigerPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Ujumbe  huo , ambao  kwa  sasa  unafikia  wafanyakazi 120 wa  Umoja  wa  Ulaya  na  wafanyakazi  kutoka katika  mataifa  ya  eneo  hilo, uliundwa  na Umoja  wa  Ulaya mwaka  2012 kufanyakazi  ya  kutoa  mafunzo kwa  polisi  ya  Niger pamoja  na  maafisa  wengine  wa  usalama  ambao  jukumu  lao  ni  kupambana  na ugaidi na  uhalifu  wa  kupangilia  katika  kanda  hiyo.

"Ningependa kwanza kuwashukuru kwa kuwa  katika  ujumbe huu, kwasababu kwanza ni maalum . Ujumbe huu  ni mgumu  na  bila  shaka  ni  wa  hatari sana kwa  jeshi la  Ujerumani."

Kabla  ya  kurejea  nyumbani  mjini  Berlin, Merkel alitarajiwa  kufanya  ziara  katika  shirika  la kupigania  haki za  binadamu  la  wanawake lililoundwa  mwaka 1998  kuwalinda  wanawake  na  watoto dhidi  ya  matumizi ya  nguvu  majumbani.

Merkel  ametoa tuzo kwa  ajili ya  usawa  wa  jinsia  iliyotolewa  kwake  na  serikali  ya  Finland kwa  shirika hilo, ambalo litatumia  euro 150,000 za  tuzo  hiyo  kujenga  makaazi  kwa  wanawake  mjini  Niamey.

Niger Kanzlerin Merkel auf Afrikareise | Merkel und Premierminister Brigi Rafini
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akisalimia na waziri mkuu wa Niger Brigi RafiniPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Ziara  hiyo  ambayo  ilimfikisha  pia  nchini  Burkina Faso na Mali  ilimalizika  leo  mjini  Niamey, ambapo serikali  ya  Ujerumani  ilikuwa  inataka  kutumia  ziara  hiyo  ya  mataifa  ya  Afrika kama sehemu  ya kulinyooshea  mkono bara  hilo  kutokana  na  maafa  baada  ya  mzozo  wa  uhamiaji.

Ujerumani yataka kusaidia ulinzi

Merkel amekwenda  katika  ziara  hiyo  akiwa na  vivutio  kadhaa  kusaidia  serikali  ya  rais  wa  Niger Mahamadou Issoufou, ili  kuimarisha  nchi  yake  yenye  matatizo.

Miongoni  mwa  ahadi  alizotoa ni  pamoja  na  kupanua mpango  wa  kuwahamisha  wakimbizi  wa kutoka Eritrea  na  Somalia , mpango  ambao  unatekelezwa  kwa  ushirikiano na  shirika  la  Umoja  wa  Mataifa  la kuwahudumia  wakimbizi  UNHCR.

Kama  sehemu  ya  mpango  huo, wakimbizi ambao  wamekwama  nchini  Libya  wanapelekwa  nchini  Niger , ambapo  kutoka  hapo  wanapelekwa  nchini  Ujerumani.

Niger Kanzlerin Merkel auf Afrikareise | Merkel und Präsident Issoufou
Kansela Angela Merkel katika mkutano na waandishi habari pamoja na mwenyeji wake rais Mahamadou IssoufouPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Ujerumani  pia  inataka  kusaidia  maendeleo  ya  kijamii  na  kijeshi  nchini  Niger, msisitizo  ukiwa  katika kuleta  hali  bora  ya  utoaji  wa  huduma  ya  afya, mipango ya  uzazi  na  elimu. Kansela  pia  amesisitiza ukweli  kwamba  kuleta  hali  bora  ya  usalama hakuwezi kufanikishwa  kwa  njia  za  kijeshi  pekee.

Merkel  alikwenda  siku  ya  Alhamis  nchini  Mali  akitokea  Burkina  Faso  ambako  alitetea  sera ya Ujerumani  ya kujizuwia  kuyauzia  silaha  mataifa  ya  eneo  hilo.  Merkel  amesema  kuna  hatari  kwamba magaidi  wanaweza  kukamata  silaha  zilizoletwa  kusaidia  mataifa  ya  Afrika  kupambana  na  ugaidi.