1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atetea sera ya wahamiaji katika kampeni

12 Machi 2016

Akiwa na shauku ya kutetea sera yake ya wahamiaji Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amejimwaga katika kampeni za mwisho katika mkesha wa "Jumapili Kabambe " katika uchaguzi wa majimbo matatu ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1ICDA
Kansela Angela Merkel katika kampeni za uchaguzi wa majimbo Baden-Württemberg. (12.03.2016)
Kansela Angela Merkel katika kampeni za uchaguzi wa majimbo Baden-Württemberg. (12.03.2016)Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Wahamiaji ni kipimo muhimu katika uchaguzi wa majimbo hayo matatu ambao unaweza kumdhoofisha kisiasa. Majimbo hayo mawili yako magharibi mwa Ujerumani na moja liko mashariki huku watu wengi wakiwa na wasi wasi vipi Ujerumani itaweza kuushughulikia mzozo huo wa wahamiaji ambapo wahamiaji milioni moja wameshuhudiwa wakiwasili nchini Ujerumani mwaka jana.

Chama cha kihafidhina cha Merkel (CDU) kimekuwa kikipoteza kuungwa mkono kwake kutokana na kupingwa kwa wahamiaji.Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) kimenufaika kutokana na hasira ya umma kuhusu wahamiaji kufuatia uamuzi wake wenye hatari kubwa wa kufunguwa mipaka ya Ujerumani kwa wakimbizi wanaokimbia vita nchini Syria.

"Kuna hali katika maisha na hii ndivyo ilivyokuwa katika kipindi cha mapukutiko kilichopita wakati unaposhindwa kuwa na mdahalo kuhusu kanuni." amesema Merkel Jumamosi (12.03.2016) akitetea uamuzi wake huo.Ameuambia mkutano wa hadhara wa chama chake cha (CDU) huko Baden- Wuettemberg mojawapo ya majimbo matatu yanayopiga kura Jumapili.

Afd chajititimua

Tayari kikiwalikishwa katika mabunge matano ya majimbo kati ya majimbo 16 ya Ujerumani chama cha AfD kimejiandaa kupata uwakilishi wa majimbo matatu zaidi kwa kutumia kauli mbiu yao ya kampeni kama vile "Linda mipaka!Komesha vurugu za watafuta hifadhi!"

Frauke Petry kiongozi wa chama cha AfD.
Frauke Petry kiongozi wa chama cha AfD.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Merkel ambaye yuko madarakani tokea mwaka 2005 na anakabiliwa na uchaguzi wa shirikisho mwakani anajaribu kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa Ulaya kukomesha wimbi la wakimbizi.Amewashtuwa viongozi wengi wa Ulaya katika mkutano wa kilele wiki hii kwa kuchezea kamari dakika za mwisho rasimu ya makubaliano na Uturuki kuzuwiya wimbi hilo la wakimbizi kwa kutaka wamuunge mkono.

Katika mkutano wa hadhara wa Baden- Wuerttenberg ambapo mgombea wa CDU yuko nyuma ya waziri mkuu wa chama cha Kijani anayetetea kiti chake kwa mujibu wa maoni ya uchunguzi, amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatumia muda mkubwa kuzungumzia makubaliano na Uturuki na kwamba uamuzi huo ni wa busara wenye kubana gharama.

Amesema huku akishangiliwa "Ndio sababu nafikiri jambo hilo ni sahihi kabisa."

Umuhimu wa makubaliano na Uturuki

Merkel inabidi afanikishe makubaliano hayo na Uturuki na viongozi wa Umoja wa Ulaya wakati wa mkutano wa ujao wa kilele hapo Machi 17 na 18.Atakwenda katika mkutano akiwa maedhoofika iwapo chama chake kitashindwa kufanya uzuri katika chaguzi hizo za majimbo.

Wahamiaji mpakani mwa Ugiriki na Macedonia,.
Wahamiaji mpakani mwa Ugiriki na Macedonia,.Picha: Reuters/S. Nenov

Huko Baden- Wuerttenberg ngome ya CDU kwa zaidi ya miaka 40 kabla ya kutiwa mikononi na muungano unaongozwa na chama cha Kijani na SPD baada ya maafa ya nyuklia huko Fukushima nchini Japani hapo mwaka 2011 waziri mkuu kutoka chama hicho cha Kijani anatazamiwa kumshinda mpizani wake wa CDU.

Katika jimbo la Saxony- Anhalt mashariki mwa Ujerumani CDU kinatarajiwa kuendelea kuwa chama kikubwa lakini uchunguzi wa maoni unaonyesha chama cha AfD kikiungwa mkono hadi asilimia 19 na mbele ya chama cha (SPD) mshirika wa Merkel katika serikali ya mseto nchini Ujerumani.

Rhineland-Palatinate jimbo lenye kupanda zabibu kwa ajili ya mvinyo linahesabiwa kuwa bado halikuamuwa kura zake watampa nani.Julia Kloechner malkia wa zamani wa mvinyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye anajiweka katika nafasi ya kumrithi Merkel siku moja umashuhuri wake umeshuka na uchunguzi wa maoni umeonyesha yuko nyuma nyuma chupu chupu ya mgombea wa SPD Malu Dreyer.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Sudi Mnette