1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel azungumzia biashara na haki za binaadamu Mexico

Mohamed Dahman
11 Juni 2017

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema amezungumza na Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto juu ya masuala mawili nyeti kabisa mbali na biashara ambayo ni mauaji ya waandishi wa habari na kutoweka kwa watu nchini humo.

https://p.dw.com/p/2eS2q
Mexiko Enrique Pena Nieto und Bundeskanzlerin Angela Merkel in Mexiko-Stadt
Picha: Reuters/C. Jasso

Kiongozi huyo wa Ujerumani  amesema amefurahi kusikia juu ya hatua zinazochukuliwa kuwalinda waandishi wa habari ambapo hadi sasa waandishi sita wameuwawa mwaka huu.

Katika mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari hapo Ijumaa (09.06.2017)katika mji wa Mexico City Merkel amesema hatarajii kucheleweshwa kwa mzungumzo ya kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kutokana na matokeo ya uchaguzi yasiotarajiwa katika uchaguzi mkuu wa Uingereza.

Katika mazungumzo hayo Merkel ameiunga mkono Mexico kushinikiza mazungumzo mapya ya mafanikio ya Makubaliano ya Biashara Huru ya Amerika Kaskazini (NAFTA) na Rais wa Marekani Donald Trump kwa kuishukuru serikali yake kwa kuzingatia maslahi ya Ujerumani wakati wa mazungumzo hayo.

Mvutano wa biashara

Mexiko Enrique Pena Nieto und Bundeskanzlerin Angela Merkel in Mexiko-Stadt
Rais Mexiko Enrique Pena Nieto na Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/H. Romero

Ujerumani na Marekani zimekuwa zikifuata sera zenye kulenga usafirishaji nje wa bidhaa zao na nchi hizo zote mbili zimekuwa na ziada ya biashara ya zaidi ya dola bilioni 60 na Marekani hapo mwaka jana.

Makampuni makubwa kabisa ya Ujerumani yana viwanda vyao nchini Mexico halikadhalika Marekani yakiwemo yale ya kutengeneza magari kama vile Volkswagen,BMW na Daimler.Hata hivyo mvutano kuhusu biashara umeibuka chini ya Rais Donald Trump na sera yake ya "Marekani kwanza."

Akidai kwamba faida wanazopata kunazigarimu kampuni za Marekani,Trump mara kwa mara amekuwa akizishambulia Mexico na Ujerumani kutokana na ziada yao ya biashara.

Na ameapa kujitowa kujitowa katika makubaliano ya biashara ya NAFTA iwapo atashindwa kuzungumzia upya makubaliano hayo kwa kuipendelea Marekani.

Akizungumza ikiwa ni wiki chache tu baada ya waziri wake wa mambo ya nje Sigmar Gabriel kuitembelea nchi hiyo na kuumga mkono msimamo wake wa kuunga mkono makubaliano ya NAFTA ,Merkel amesema amefurahishwa na nchi zilizosaini makubaliano hayo za Marekani, Mexico na Canada kuzungumzia kuyarefusha makubaliano hayo.Amesema anataraji mazungumzo hayo yatakuwa ya mafanikio.

Ongezelo la biashara na Ulaya

Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto amemwambia Kansela Merkel anataka ongezeko kubwa la biashara na Umoja wa Ulaya akiahidi kukamilisha makubaliano mapya ya biashara kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Serikali yake imekuwa ikitafuta fursa mpya za kibiashara tokea Rais Trump aingie madarakani na kitisho cha kudhibiti upendeleo wa Mexico kupata nafasi katika masoko ya Marekani.

Mexico hivi sasa iko mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuyafanya makubaliano ya biashara huru waliyosaini miaka 20 iliopita kuwa ya kisasa.Viongozi wote wawili Merkel na Pena Nieto wameahidi kukamilisha makubaliano hayo yatakyokuwa yametanuliwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Kujitolea kwa Mexico

Merkel amepongeza kujitolea madhubuti kwa Mexico katika biashara huru ikiwa kama ni kijembe mashambulizi ya Trump dhidi ya utandawazi.Mwezi uliopita Trump pia alishambulia kile alichokiita nakisi kubwa mno ya bishara ya Marekani iliyonayo na Ujerumani  na kuishutumu nchi hiyo kwa kushindwa kulipia mchango wake kwa Jumuiya Kujihami ya NATO.

Mexico na Ujerumani mwaka jana zimefanya bishara yenye thamani ya dola bilioni 1.7 na zina shauku ya kutanuwa uhusiano wao.Uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja wa Ujerumani nchini Mexico umefikia jumla ya dola bilioni 2.4 mwaka jana kuliko nchi nyengine yoyote ile ziada ya Marekani na Uhispania.

Merkel ambaye anaandamana na ujumbe mkubwa wa wafanya biashara awali alikuwa nchini Argentina taifa jengine lenye nguvu kubwa za kiuchumi Marekani ya Kusini hapo Alhamisi na Ijumaa asubuhi.

Jumamosi anatarajiwa kuhudhuria jukwaa la kiuchumi kabla ya kurudi nyumbani Ujerumani.

Mwandishi :Mohamed Dahman/AFP/Reuters/dpa

Mhariri : Caro Robi