1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel azuru Uhispania baada ya makubaliano ya wakimbizi

Sekione Kitojo
12 Agosti 2018

Kansela  Merkel amesema nchi yake inaunga mkono juhudi za Uhispania za kuzuwia mmiminiko wa wakimbizi  kutoka Morocco kwenda Ulaya kupitia bahari ya Mediterania, siku kadhaa baada kutia saini makubaliano ya wakimbizi.

https://p.dw.com/p/331X6
Merkel trifft Spaniens Premier Pedro Sanchez
Picha: Reuters/M. del Pozo

Akizungumza baada  ya  kuwasili  siku  ya  Jumamosi katika  mji  wa San Lucar de Barrameda  kusini  mwa  Uhispania  kwa  mazungumzo na  waziri  mkuu  mpya  wa  nchi  hiyo, Pedro Sanchez , Merkel amesema  kwamba  Uhispania ilikuwa  inaongoza  majadiliano  na nchi  jirani  yake ya  Afrika  kaskazini.

Merkel trifft Spaniens Premier Pedro Sanchez
Angela Merkel(kushoto) akisalimiana na mwenyeji wake waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez.Picha: Reuters/M. del Pozo

Ushirikiano  wa ukweli na  mataifa  ya  Afrika  ni  muhimu kuweza kupata  kurejeshwa  kwa  waombaji  hifadhi  ambao  wamekataliwa, aliongeza.

Uhispania , "imo  katika  mbinyo  mkubwa  wa  wakimbizi  wanaotoka katika  mataifa  ya  kusini mwa  jangwa  la  Sahara," Sanchez amesema.

Merkel  ameongeza  kwamba  makubaliano  na  mataifa  ya  Afrika ya  wanakotoka  wakimbizi  pamoja  na  nchi  wanakopitia yatafanya kazi "pale  tu wakati  pande  zote  mbili  zitakapopata  kitu  kutokana na  hali  hiyo, tunaweza  tu  tukazungumza  kuhusu  Afrika, tunapaswa  kuzungumza  na  Afrika," amesema.

Sanchez  na  mkewe, Begona Gomez, walimlaki Merkel  na  mume wake, Joachim Sauer, mapema  mchana, mwanzoni  mwa  ziara  ya siku  mbili  ambamo  suala  la  uhamiaji  linatarajiwa  kuwa  ajenda muhimu.

Merkel trifft Spaniens Premier Pedro Sanchez
Merkel na mumewe (katikati) wakiwa na waziri mkuu Pedro Sanchez (kulia) na mkewe Begona Gomez(kulia)Picha: picture alliance/dpa/E. Briones

Siku  ya  Jumatatu, Ujerumani  na  Uhispania  zilifikia makubaliano kuwarejesha  Uhispania  wahamiaji  wanaowasili  nchini  Ujerumani katika  muda  wa  masaa  48 iwapo  bado  wana maombi  ya kuomba  hifadhi  ambayo  hayajakamilika nchini  humo.

Makubaliano na nchi nyingine za Ulaya

Uhispania  ni  nchi  ya  kwanza  katika  Umoja  wa  Ulaya kutia  saini makubaliano  kama  hayo  na  Ujerumani.

Alipoulizwa  iwapo  makubaliano  hayo  ni  ishara  tu , kutokana  na kwamba  waombaji  wachache   wa  hifadhi  wanawasili  nchini Ujerumani  baada  ya  kuorodheshwa  nchini  Uhispania, Merkel alisema  kwamba  inaonesha, "kwamba Ujerumani  na  Uhispania zinaunga  mkono  suluhisho  la  Ulaya "  katika  suala  la  uhamiaji.

Merkel  ana  matumaini  ya  kupata  makubaliano  kama  hayo  na Ugiriki  na  Italia  baada  ya msuguano  mkubwa  kuhusu  sera  za uhamiaji na  waziri  wake  wa  mambo  ya  ndani  Horst  Seehofer ambao  ulitishia  kuiangusha  serikali  yake  ya  muungano  mapema mwezi  Julai.

Mzozo  huo ulishuhudia  Merkel  akiahidi  hatua ambazo  waombaji hifadhi  ambao  tayari wameandikishwa  kwingine  katika  mataifa  ya Umoja  wa  Ulaya wakirejeshwa  katika  taifa  ambalo  walijiandikisha kwanza kuomba  hifadhi.

Merkel trifft Spaniens Premier Pedro Sanchez
Merkel(kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mkuu Pedro Sanchez(kulia)Picha: Reuters/M. del Pozo

Pamoja  na  uhamiaji, viongozi  hao  wawili  wanatarajiwa  kujadili mageuzi  ya  kiuchumi  na  fedha  katika  Umoja  wa  Ulaya , mkutano wa  kilele  wa  hivi  karibuni  wa  NATO  na  ulinzi  katika  Umoja  huo.

Pia  alipangiwa   kufanya  ziara  katika  mbunga  ya  taifa  iliyoko karibu  na  hapo  ya  Donana, kwa  mujibu  wa  msemaji  wa  serikali ya  Ujerumani  siku  ya  Jumamosi. Kwa mujibu  wa  tarakimu  kutoka katika  shirika  la  kimataifa  la  uhamiaji , Uhispania imekuwa  lengo jipya  la  wahamiaji  kutoka  bara  la  Afrika. Wengi  wao  wanatoka Morocco kupitia  ujia  wa  Gibraltar , karibu  kilometa  14  tu  katika eneo  lake  la  karibu, ama  katika  bahari  ya  Alboran  iliyoko katikati  ya   rasi  ya  Iberia na  Afrika  kaskazini.

Kuanzia  Januari  hadi  mwishoni  mwa  Julai, zaidi  ya  watu  23,000 waliingia  Uhispania  kupitia  bahari  ya  Mediterania , wastani  wa mara  tatu  katika  kipindi  kama  hicho  mwaka  jana.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae

Mhariri: Jacob Safari