1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Hollande waijadili Misri

16 Agosti 2013

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wanazungumza juu ya mgogoro wa Misri, huku nchini Misri kwenyewe nchi ikijiandaa kwa maandamano makubwa yaliyopewa jina la "Ijumaa ya Hasira".

https://p.dw.com/p/19QuD
German Chancellor Angela Merkel attends a Christian Democratic Union (CDU) election campaign rally in Seligenstadt near Frankfurt August 14, 2013. Returning from a three week vacation, Merkel officially launched her campaign in Seligenstadt near Frankfurt and for a third term as leader in September's election. REUTERS/Ralph Orlowski (GERMANY - Tags: POLITICS ELECTIONS)
Wahlkampf Angela Merkel in SeligenstadtPicha: Reuters

Mazungumzo hayo yanayofanyika mchana huu kati ya Merkel na Hollande, yanafuatia onyo la hapo jana la Hollande kwamba Misri inaelekea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Serikali zote mbili ziliwaita mabalozi wanaoiwakilisha Misri, kama zilivyofanya pia nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya, kwa lengo la kulaani mauaji hayo makubwa kabisa kuwahi kutokezea kwa siku moja kwa wakati mmoja ndani ya historia ya karibuni ya dunia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amekiambia kituo cha redio cha RTL hivi leo kwamba hali ya Misri inatisha sana, na ni hatari kwa eneo zima la Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiarabu.

Fabius ameonya kwamba makundi yenye siasa kali yanaweza kutumia fursa ya sasa ya machafuko kujipenyeza na kuigeuza kabisa taswira ya mgogoro huo.

Umoja wa Mataifa walaani mauaji

Jumuiya ya kimataifa imeendelea na kuyalaani mauaji hayo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha mkutano wa dharura juu ya mgogoro huo kwa ombi la Ufaransa, Uingereza na Australia.

Maiti za mauaji ya Jumatano zikianza kuzikwa mjini Cairo.
Maiti za mauaji ya Jumatano zikianza kuzikwa mjini Cairo.Picha: Reuters/Steve Crisp

Balozi wa Argentina kwenye Umoja wa Mataifa, Maria Cristina, ambaye nchi yake ndiyo rais wa sasa wa Baraza la Usalama, amesema wajumbe wa Baraza hilo wamesikitishwa na kiwango cha mauaji mjini Cairo, na kutoa wito wa kusitishwa kwa ghasia na haja ya kuwepo kwa muafaka wa kitaifa.

Wakati hayo yakiendelea, Uturuki imesema kwamba balozi wake nchini Misri anarudi nyumbani hivi leo, baada ya nchi zote mbili kuwaita mabalozi wao kufuatia mauaji hayo ya Jumatano. Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kimataifa kuyalaani vikali mauaji hayo, akiyaita "mauji ya maangamizi".

Serikali ya Uturuki ilikuwa ikimuunga mkono Mohamed Mursi kama kiongozi wa kwanza wa Kiislamu kuchaguliwa kidemokrasia kwenye ulimwengu wa Kiarabu, na imekuwa ikiyakosoa vikali mapinduzi ya kijeshi ya Julai 3, yaliyomuondoa madarakani Mursi.

"Ijumaa ya Hasira"

Nchini Misri kwenyewe, ambako picha za namna mauaji ya Jumatano yalivyotokea zimeanza kusambaa mitandaoni na kwenye televisheni za kimataifa, kundi la Udugu wa Kiislamu limeitisha kile linachokiita "Ijumaa ya Hasira", huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa pande zote kuonesha uvumilivu.

Maandamano ya awali yaliyoandaliwa na Tamarod kupinga utawala wa Mursi.
Maandamano ya awali yaliyoandaliwa na Tamarod kupinga utawala wa Mursi.Picha: Hamlet Tajarod

Tayari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imeshasema kwamba vyombo vya usalama vitatumia risasi za moto dhidi ya mtu yeyote atakayeelekeza mashambulizi yake kwenye majengo ya serikali.

Msemaji wa Udugu wa Kiislamu, Gehad al-Haddad, ametangaza kupitia mtandao wa Twitter, kwamba "maandamano dhidi ya mapinduzi ya kijeshi yataanza kwenye misikiti yote ya Cairo kuelekea kwenye uwanja wa Ramsis baada ya sala ya Ijumaa."

Laila Moussa, msemaji wa Muungano dhidi ya Mapinduzi ya Kijeshi, amesema maandamano kama hayo yamepangwa kufanyika nchi nzima. Amesema wafuasi wa Mursi, wakiwemo wabunge wawili wa zamani, wamekamatwa alfajiri ya leo na vyombo vya usalama.

Hapo jana, kundi la Tamarod, ambalo ndilo lililoratibu upinzani dhidi ya utawala wa Mursi, pia limewataka Wamisri kuingia mitaani leo, kupinga kile linachokiita "ugaidi na uingiliaji wa kigeni".

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/DPA
Mhariri: Saumu Yussuf