1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Hollande wapania makubaliano thabiti ya tabianchi

Admin.WagnerD19 Mei 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francoise Hollande wameahidi kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa makubaliano thabiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi yanafikiwa mwaka huu mjini Paris, Ufaransa.

https://p.dw.com/p/1FSnr
Deutschland 6. Petersberger Klimadialog in Berlin
Picha: Reuters/T. Schwarz

Kansela Merkel na Rais wa Hollande walishiriki katika mkutano wa kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira siku ya Jumanne (19.05.2015), katika maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika baadae mwaka huu mjini Paris.

Wakiwahutubua mawaziri wa mazingira mjini Berlin, Angela Merkel na Francoise Hollande, viongozi wa mataifa mawili yenye uchumi mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya, walizitaka nchi nyingine kutimiza wajibu wao katika kusaidia kupunguza utoaji wa gesi chafu.

Walisema Ujerumani na Ufaransa zimeamua kwa dhati kufanya kila juhudi ili kufikia makubaliano thabiti, mapana na yenye kufungamanisha ya Umoja wa Mataifa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

"Na katika ushirika wa Ujerumani na Ufaransa tunalenga kufanya kila kitu kwa ngazi ya wizara na pia kwa ngazi ya wakuu wa nchi ili kuufanya mkutano huu (wa Paris) kuwa wa ufanisi. Ni suala la 'fanya tu hivyo' na kila moja mwenye kufuatilia jambo hili anajua hili linamaanisha nini, kwamba tutafikia makubaliano yanayofungamanisha," alisema Merkel.

Hollande na Merkel wakihutubia mkutano wa Petersberg Klimadialog mjini Berlin siku ya Jumannne.
Hollande na Merkel wakihutubia mkutano wa Petersberg Klimadialog mjini Berlin siku ya Jumannne.Picha: Reuters/F. Bensch

Alisema Ujerumani inalenga kuongeza maradufu ufadhili wake wa mazingira kufikia mwaka 2020 ikilinganishwa na mwaka 2014, kwa kuongeza msaada kutoka bajeti ya sasa ya euro bilioni 4 kila mwaka, na kuongeza fedha zilizopo kwenye benki ya taifa ya maendeleo KfW hadi kufikia euro bilioni 3.

Ahadi ya matajiri

Mataifa tajiri yameahidi ifikapo mwaka 2010, yawe yanachangia dola bilioni 100 kila mwaka za ufadhili wa mazingira, ambazo ni nyongeza ya ufadili uliyopo tayari. Lakini mpaka sasa ni dola bilioni 10 tu zilioahidiwa. Merkel amesema ni muhimu kwamba miradi ya kwanza ya maendeleo ya mazingira inaanzishwa kabla ya Mkutano wa Paris.

Mazungumzo hayo yamefanyika chini ya mpango wa "Majadiliano ya tabianchi wa Petersberg", ulioanzishwa na Merkel mwaka 2010, kujiandaa na Mkutano wa Mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa mjini Paris mwezi Desemba mwaka huu.

Hollande apania kufikia lengo la nyuzi mbili

Rais Francoise Hollande ameweka lengo lenye tamaa kwa mkutano wa Paris -- ambalo ni makubaliano ya kupunguza kupanda kwa joto la dunia linalohusishwa na utoaji wa gesi chafu kwa hadi nyuzi joto mbili za celsius kutoka viwango vya kabla ya maendeleo ya kiviwanda.

"Ikiwa makubaliano yatafikiwa, laazima yawe ya dunia nzima. Ndiyo kusema, laazima yatumike kwa kila mmoja. Laazima yawe makubaliano ya muda mrefu," alisema rais Hollande.

Wana Ekolojia kadhaa walipiga kelele za "Sitisha makaa ya mawe, linda mazingira" wakati Merkel na Hollande wakiwasili kwenye mkutano huo katikati mwa mji wa Berlin, uliohudhuriwa na wawakilishi wa mataifa 35, ambao ulianza siku ya Jumatatu.

Waandamanaji wa shirika la Green Peace wakionyesha vikaragosi vya Hollande, Merkel na rais wa Marekani Barack Obama.
Waandamanaji wa shirika la Green Peace wakionyesha vikaragosi vya Hollande, Merkel na rais wa Marekani Barack Obama.Picha: T. Schwarz/AFP/Getty Images

Shirika la mazingira la Green Peace lilisimamisha ruwaza ya futi 20 ya Mnara wa Eiffel ulioguuzwa kuwa mtambo wa kufua umeme kwa kutumiam upepo karibu na lango la Brandenburg, kutoa wito wa kutumia vyanzo jadidifu tu vya umeme kufikia mwaka 2050.

Merkel ataka makubaliano ya haki

Pamoja na kutihibitisha shabaha ya nyuzi joto mbili, Merkel amesema makubaliano mapya ya kimataifa kuhusu tabianchi lazima yaweke sheria za haki na zinazofungamanisha kwa mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea, yahamasishe uwekezaji wa kijani na kusaidia mataifa maskini, ikiwemo kujirekebisha kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Sote tunaweza kuikabili changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwa tunaweza kuwa na imani kwamba washirika wetu wa kimataifa watafuata lengo sawa," Merkel aliwambia wajumbe wa mkutano wa Berlin.

Ujerumani ambayo imeahidi kuachana kabisaa na matumizi ya nishati ya nyuklia na mafuta ya ardhini na kuimarisha vyonzo jadidifu chini ya programu yake ya mpito wa nishati, imefanya ulinzi wa mazingira kuwa suala kuu la urais wake wa kundi la mataifa saba yalioelndelea zaidi kiviwanda duniani G7 kwa mwaka huu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman