1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kuanza ziara Marekani

Sekione Kitojo
26 Aprili 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kuanza ziara rasmi ya siku moja nchini Marekani kukutana na rais Donald Trump  katika mazungumzo muhimu yatakayotuwama katika kuokoa makubaliano ya kinyuklia na Iran.

https://p.dw.com/p/2wk1L
Trump schüttelt Merkel nicht die Hand
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kansela  Angela  Merkel  anakabiliwa  na  mtihani  wake  mkubwa kufuatia mwanzo ambao  haukuwa  mzuri  katika  muhula  wake mpya  madarakani  akiwa  kama mkuu  wa  taifa  lenye  uchumi mkubwa  barani  Ulaya  wakati  atakapokutana  na  rais  wa Marekani  Donald  Trump  leo  katika  juhudi  zake  za  kuonesha mamlaka  ya  kisiasa  ya  Ujerumani  mjini  Washington.

Pressekonferenz von Kanzlerin Merkel und Premierminister Ardern
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture alliance/AA/C. Karadag

Biashara  itakuwa  mada  muhimu  ya  majadiliano  katika  mkutano wa  viongozi  hao  wawili, kabla  ya  msamaha  wa  ushuru  wa forodha  katika  bidhaa  za  chuma  na  bati   uliotolewa  kwa  Umoja wa  Ulaya  kumalizika  muda  wake  hapo  Mei  mosi.

"Kwa mtazamo  wa  hivi  sasa, mtu  anapaswa  kutarajia  kwamba ushuru  utaanza  Mei mosi,"  afisa  mmoja  alisema, akisisitiza kwamba  Ujerumani  itaendelea  na  majadiliano  kuhusiana  na suala  la  biashara  na  kujaribu  kufikia  makubaliano  mapana  zaidi katika  viwanda.

"Tunataka  kujadili  ushuru wa  viwanda  kwa  jumla," afisa  huyo amesema, akidokeza  kwamba, "Kuna  tofauti  fulani  ndani  ya Umoja  wa  Ulaya."

USA PK US-Präsident Trump und französicher Präsident Macron in Washington
Rais Donald Trump akizungumza wakati wa ziara ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini WashingtonPicha: Reuters/K. Lamarque

Ziara  ya  siku  moja  ya  Merkel  inafuatia  ziara  ya  siku  tatu  mjini Washington iliyofanywa  na  rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron.

Merkel kumshawishi Trump kuhusu  Iran

Macron  aliitaka  Marekani  kutoachana  na  makubaliano  ya kimataifa  ya  kinyuklia  na  Iran wakati  mabalozi  wa  mataifa  ya magharibi  wamesema  Uingereza, Ufaransa  na  Ujerumani wanakaribia  kufikia  makubaliano  ambayo  yanataka  kumshawishi Trump  kuokoa mkataba  huo.

Trump  ameueleza  mkataba  huo  wa  mwaka  2015, ambao  Iran imekubali  kuzuwia shughuli  zake  za  kinyuklia ili  kuweza  kupata kuondolewa  vikwazo  vya  kiuchumi, kuwa  ni  makubaliano  mabaya kabisa  kuwahi  kujadiliwa  na  ametishia  kuyavunja  kwa  kurejesha vikwazo  vya  Marekani  mwezi  ujao, iwapo  washirika  wake  wa Ulaya  hawatakubali  kuutengeneza  upya  kurekebisha  mapungufu yake.

Pamoja  na  hayo ziara  ya  Merkel  nchini  Marekani  inakuja  huku kukiwa  na  hatari  kwa  kansela  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  63, ambaye  amekuwa  na  mwanzo  mbaya  katika  uhusiano  wake  na Trump.

USA Washington - Donald Trump trifft Emmanuel Macron - Gala
Ziara ya Emmanuel Macron nchini Marekani ilikuwa ya mvuto mkubwa kwa viongozi haoPicha: Getty Images/C. Kleponis

Hii  imekuja  baada  ya  Trump  kuushambulia  vikali msimamo  wa kiliberali  wa  Merkel  kuhusu  wakimbizi  katika  kampeni  yake  ya urais  mwaka  2016, akiueleza  kuwa  ni  maafa, na  kutaka serikali ya  Ujerumani  ipunguze nakisi  yake  kubwa  ya  biashara  na Marekani  pamoja  na  kuongeza mchango  wake  katika  jukumu  la kuiendesha  jumuiya  ya  NATO.

Ziara muhimu kwa Merkel

Merkel  ambaye  huchukua  tahadhari  mno ameshindwa kutengeneza  uhusiano  wa binafsi  na  Trump na  hali  ya  ziara yake  katika  Ikulu  ya  Marekani  ya  White House  bila  shaka itatofautiana  kwa  kiasi  kikubwa  na  ziara  ya  Macron  iliyokuwa na  mvuto  mkubwa  wa  mapenzi  kwa  viongozi wote  wawili.

Bundeskanzlerin Merkel mit US-Präsident Trump
Uhusiano kati ya Merkel na trump haujawa mzuri sanaPicha: AFP/Getty Images/L. Marin

"Kansela  anafurahia  ziara  hii kwasababu  anaamini   katika uhusiano  kati  ya  Marekani  na  Ulaya,"   mmoja  kati  ya  maafisa alisema. "Ni muhimu kujenga  uhusiano  huu."

Mtaalamu  wa  uchumi  katika  benki ya  ING  nchini  Ujerumani Carsten  Brzeski,  amesema  kwamba  "ziara  ya  Merkel itawakilisha  fursa  ya  kwanza  kwa  kansela  huyo  kuona  iwapo Marekani  bado  inamuona  kuwa  ni  kiongozi  mkuu  wa  Ulaya."

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / dpae / rtre

Mhariri: Josephat Charo