1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU chafanya kongamano la siku mbili

Caro Robi14 Desemba 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atawahutubia wanachama wa CDU katika juhudi za kuwaunganisha baada ya kuwepo tofauti miongoni mwao kutokana na msimamo wake wa kuwapokea maelfu ya wahamiaji nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1HMtG
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Kongamano la siku mbili la chama cha CDU linalofaniyka katika mji wa kusini magharibi mwa Ujerumani wa Karslruhe unalenga kufikia mtizamo wa pamoja kuhusiana na suala la wahamiaji baada ya wiki kadhaa za kuvutana miongoni mwa wanachama wa chama hicho na ikiwa imesalia miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi wa majimbo kadhaa muhimu.

Ujerumani inatarajiwa kupokea wahamiaji milioni moja ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kupokewa na nchi ya Ulaya. Kuwasili kwa wahamiaji wapya kumemfanya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kushinikizwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na mzozo huo hasa ndani ya chama chake mwenyewe.

Wahamiaji ndiyo mada kuu

Zaidi ya wajumbe 1,000 watamsikiliza Merkel akitetea sera zake kuhusu suala hilo la wahamiaji ambapo ametakiwa kuchukua hatua madhubuti kupunguza mmiminiko wa wahamiaji lakini wakati huo huo kuacha milango wazi kwa wanaotoroka vita na machafuko nchini mwao.

Kansela wa Ujerumani Angel Merkel na baadhi ya wanachama wa CDU mjini Karlsruhe
Kansela wa Ujerumani Angel Merkel na baadhi ya wanachama wa CDU mjini KarlsruhePicha: Reuters/R. Orlowski

Hapo jana Merkel alisema bila shaka watakuwa na mjadala wa kina kuhusu suala hilo katika kongamano hilo la CDU kwani ndilo jambo ambalo Ujerumani nzima inalizungumzia.

Kansela huyo wa Ujerumani hata hivyo amesema kwake ni muhimu sana kusema kuwa watatekeleza wajibu wao wa kibinadamu na wajibu wao kwa Ulaya.

Merkel na chama chake ambacho amekiongoza kwa miaka 15 watatoa azimio kuhusu suala hilo la mzozo wa wahamaji ambalo litapigiwa kura baada ya hotuba yake ambayo wachambuzi wanasema itakuwa kama kura ya maoni kuhusu utawala wake.

Huku wahamiaji na wakimbizi wakizidi kumiminika Ujerumani hata wakati huu wa msimu wa baridi kali,wajerumani wanamtaka Merkel mwenye umri wa miaka 61 kutoa muongozo bayana kuhusu ni namna gani atalishughulikia suala hilo.

CDU Bado imara

Wanachama wa CDU wanatiwa wasiwasi na msimamo wa kiongozi wao huku chaguzi za majimbo matatu muhimu zikitrajiwa mwezi Machi mwakani ambapo kutokana na manung'uniko miongoni mwa raia huenda chama cha mrengo wa kulia cha AFD kikapata uungwaji mkono zaidi ambacho kulingana na kura za maoni kinaungwa mkono kwa asilimia 10.

Angela Merkel na Kiongozi wa CSU Horst Seehofer
Angela Merkel na Kiongozi wa CSU Horst SeehoferPicha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Hata hivyo chama cha CDU bado kinaongoza katika uungwaji mkono miongoni mwa umma kwa asilimia39 huku chama mshirika wake serikalini cha SPD kikifuata kwa asilimia 24.

Uamuzi pia unatarajiwa mwaka ujao iwapo Merkel ndiye atakayepeperusha bendera ya chama cha CDU katika uchaguzi mkuu mwaka 2017. Merkel kufikia sasa hana mpinzani ndani ya chama chake huku wakosoaji wake wakikiri kuwa kufikia sasa anasalia kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi kuweza kugombea tena wadhifa wa Kansela wa Ujerumani.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Yusuf Saumu