1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Bush wakutana kabla ya ufunguzi rasmi wa G-8

P.Martin6 Juni 2007

Ujerumani na Marekani zikijaribu kupunguza tofauti zao kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani,polisi kwa upande mwingine wanahangaika kuwazuia waandamanaji kufika mji wa Heiligendamm. Huko ndio walikokusanyika viongozi wa mataifa manane tajiri yalioendelea kiviwanda G-8 kwa mkutano utakaoendelea hadi tarehe 8 Juni.

https://p.dw.com/p/CHD4
Kansela Angela Merkel(kulia) na Rais George W.Bush wakizungumza na waandishi wa habari Heiligendamm
Kansela Angela Merkel(kulia) na Rais George W.Bush wakizungumza na waandishi wa habari HeiligendammPicha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani,ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya ni mwenyekiti wa mkutano huo wa G-8 mjini Heiligendamm,kaskazini mwa Ujerumani.Merkel, kwenye mkutano huo,ameazimia kutoa kipaumbele kwa suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Lengo lake ni kupata makubaliano kupitia Umoja wa Mataifa ambayo yatakuwa na malengo maalum ya kupunguza gesi ya kaboni dayoksaidi inayochafua mazingira pamoja na kutoruhusu ujoto wa dunia kuongezeka kwa zaidi ya nyuzi joto 2 za Celsius ifikapo mwaka 2050.

Kwa upande mwingine,Rais Bush alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Merkel alisema,ana dhamira kubwa ya kushirikiana na Merkel kupata makubaliano mapya baada ya kumalizika muda wa Mkataba wa Kyoto,juu ya njia za kupunguza viwango vya gesi inayochafua mazingira na pia kutafuta nishati mbadala. Akaongezea kuwa kuna nafasi nzuri ya kushirikiana kiteknolojia pamoja na mataifa yanayoendelea ili kuhakikisha ulinzi wa mazingira kama ipasavyo.

Lakini yadhihirika kuwa bado kuna tofauti za maoni kuhusu hatua za kuchukuliwa kupambana na ongezeko la ujoto duniani.Kwani baada ya mkutano wa Bush na Merkel,ujumbe wa Bush umesema,maazimio yatakayotolewa mwishoni mwa mkutano wa kilele wa G-8,hautojumuisha malengo ya pamoja kuhusu uzalishaji wa gesi ya kaboni dayoksaidi inayochafua mazingira.

Juu ya hivyo,Kansela Merkel amesema mada kuu mbili za mkutano huo zimechomoza katika majadiliano yao;yaani mabadiliko ya hali ya hewa na kupiga vita umasikini barani Afrika.Amesema, wamebadilishana maoni kwa kina kuhusu mada zote mbili.Anaamini kuwa watashirikiana zaidi na watapata nafasi nzuri ya kuwa na msimamo wa pamoja.Merkel akaongezea kuwa mazungumzo hayo ya mwanzo na Bush yalikwenda vizuri na yamekuwa na mafanikio.

Kwa upande mwingine Kansela Merkel akitazamia kuufungua rasmi mkutano wa kilele wa G-8 baadae hii leo katika dhifa ya chakula cha jioni, wapinzani wa mkutano huo ndio wanajaribu kuvikwepa vizuizi vya polisi kwa azma ya kukaribia eneo la mkutano.

Kwa mujibu wa polisi kama watu 10,000 walifanikiwa kujipenyeza sehemu mbali mbali.Vile vile maelfu kadhaa ya waandamanaji waliziba kwa muda barabara mbili zinazoelekea mji wa Heiligendamm.Baadhi ya wapinzani walirushiwa maji baada kuwatupia mawe polisi.Inasemekana kuwa hadi polisi wanane wamejeruhiwa.Wakati huo huo, Mahakama ya Katiba ya Ujerumani imethibitisha kuwa kwa sababu za usalama,maandamano yamepigwa marufuku karibu na uzio wa senyenge unaozunguka mahala pa mkutano.

Mbali na makundi madogo ya waandamanaji wanaofanya ghasia,baadhi kubwa wanataka kuandamana kwa amani wakitaka misaada zaidi itolewe kupiga vita umasikini barani Afrika.

Majadiliano makuu ya mkutano wa G-8 yataanza siku ya Alkhamisi na kuendelea hadi tarehe 8 Juni.