1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Macron kuujadili mpango wa uokozi wa corona

Saleh Mwanamilongo
29 Juni 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekuwa mwenyeji wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa mazungumzo, siku chache kabla ya Ujerumani kuchukua urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/3eWh2
Berlin | Angela Merkel und Emmanuel Macron
Picha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Kwa Ujerumani kuchukua uwenyekiti wa Umoja huo ulio na wanachama 27 utakuwa wa mwisho kwa Merkel kama kiongozi na uenyekiti huo huenda ukawa ndio utakaobainisha urithi wa kansela huyo wa Ujerumani aliyepewa jina la "Kansela wa milele”

Wakati uhusiano wa siku za usoni baina ya Umoja huo na Uingereza ukiwa bado haujaamuliwa, muelekeo wa kuwa na dunia yenye kiwango kidogo cha hewa chafu na uhusiano unaozidi kudorora kati ya China na Marekani, yote yakiwa muhimu kujadiliwa inaonesha kuwa hapatakuwa na ukosefu wa mada za kuzungumziwa. Lakini janga la virusi vya corona na kudhoofika kwa uchumi wa dunia ndiyo mambo yanayoonekana kupewa uzito zaidi.

Spanien Außenminister Heiko Maas in Valencia
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

"Mgogoro huu tunaoupitia ni tofauti tukilinganisha na migogoro tiliyopitia tangu kuundwa kwa Umoja wa Ulaya," alisema Kansela Angela Merkel ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 2005, katika hotuba yake bungeni akielezea mipango ya taifa lake katika jukumu la uwenyekiti wa Umoja huo.

Amesema barani Ulaya pekee janga la corona limesababisha vifo vya zaidi ya watu laki moja huku wiki kadhaa za mkwamo wa kiuchumi zikihatarisha kile ambacho Ulaya imekijenga kwa miaka mingi iliyopita.

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hata hivyo zina hamu ya kuona kile Ujerumani mwanachama aliye na uchumi mkubwa katika umoja huo itakachokifanya katika nafasi yake ya uwenyekiti. Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akizungumza na gazeti la Handelsblat la hapa Ujerumani, amesema ni bahati nzuri kwamba Ujerumani inachukua uwenyekiti katika wakati huu wa mgogoro mkubwa, na kwamba uzoefu wa Kansela Markel pamoja na uaminifu wake utasaidia pakubwa katika kujaribu kutuliza hali.

EU-Gipfel | Finanzhilfen Coronakrise | von der Leyen & Michel
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya von der LeyenPicha: Reuters/O. Hoslet

Ujerumani inachukua uwenyekiti wa Umoja huo kwa nguvu zote kutokana na kwamba imeshughulikia dharura ya kiafya vizuri zaidi kuliko mataifa mengine wanachama wa Umoja huo. Akiwa pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Merkel ametoa mpango wa dola milioni 840 zilizopendekezwa na von der Leyen ili kuupiga jeki uchumi wa Ulaya. Fedha hizo zitapewa, bila nia ya kuzirejesha, mataifa yaliyoathirika zaidi na janga la corona. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amesema wanataka kutumia janga hili kuleta mabadiliko katika Umoja wa Ulaya.

Kabla ya ziara yake mjini Berlin, Emmanuel Macron aliahidi Euro bilioni 15 kwa ajili ya mageuzi ya kiekolojia ya uchumi wa nchi yake, hatua hiyo imekuja siku moja baada ya watetezi wa mazingira kupata mafanikio makubwa kwenye uchaguzi wa manispaa jana Jumapili kote nchini Ufaransa.

"Tunatakiwa kurejesha malengo makuu ya kiekolojia kwa ajili ya uchumi endelevu," alisema Macron wakati akipopokea ripoti ya mageuzi ya mfumo wa uongozi nchini mwake kutoka kwa raia 150 aliowateuwa kufuatia maandamano ya madereva mwaka uliopita.