1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Sarkozy wasimama pamoja

7 Februari 2012

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wamekubaliana juu ya masuala yote muhimu kwenye mkutano wao mjini Paris na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao juu ya hayo.

https://p.dw.com/p/13yWm
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: picture-alliance/dpa

Mhariri wa gazeti la "Braunschweiger" anasema mkutano huo ulikuwa wa mafanikio. Sababu ni kwamba viongozi hao walikubaliana siyo tu juu ya Ugiriki bali pia walionyesha msimamo wa pamoja katika kuzipinga Urusi na China kutokana na hatua ya nchi hizo ya kuzitumia kura za turufu kulipinga Azimio la Baraza la Usalama juu ya Syria. Mhariri wa gazeti la "Brauschweiger" anasema bila ya Kansela Merkel na Rais Sarkozy kusimama pamoja, Umoja wa Ulaya unaweza kusambaratika.

Lakini mhariri wa gazeti la "Badische" anasema licha ya mabusu ya upande wa kulia na kushoto baina ya Kansela Merkel na Rais Sarkozy, kila mtu anajua kwamba bado zipo tofauti baina ya viongozi hao. Hata hivyo migogoro aghalabu huwaleta watu pamoja. Mhariri huyo anaeleza kuwa katika mgogoro wa Euro, Merkel na Sarkozy wanasonga mbele pamoja.

Mhariri huyo anauliza jee kitatokea nini ikiwa kiongozi wa chama cha upinzani Hollande atashinda katika uchaguzi? Mhariri huyo anahoji kwamba mambo yataendelea kama yalivyokuwa baina ya Makansela wa siku za nyuma na marais wa Ufaransa. Pia Merkel na Hollande watatambua umuhimu wa uhusiano baina ya nchi zao na kwa hivyo pia yatakuwapo mabusu baina yao.

Mhariri wa "Reutlinger General" Anzeiger anatilia maanani kwamba mambo yatakuwa magumu, baina ya Ujerumani na Ufaransa, ikiwa kiongozi wa upinzani Hollande atashinda katika uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa bado imebakia miezi mitatu kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa na mpinzani wa Sarkozy, Bwana Hollande anaongoza katika kura za maoni. Hayo yanaeleza sababu ya Kansela Merkel ya kushikamana na Sarkozy. Ujerumani inawiwa vigumu kumwona Hollande kuwa mshirika wake .

Sarkozy na Merkel
Sarkozy na MerkelPicha: AP

Sababu ni kwamba Hollande amewaahidi wapiga kura kwamba ataifanyia mazungumzo upya mikataba muhimu ya Umoja wa Ulaya ikiwa pamoja na ule wa bajeti ambao Kansela Merkel anautumia kama msingi wa kuutatua mgogoro wa madeni.

Gazeti la "Rhein-Necker" halikubaliani na tathmini hiyo na linauliza, kwa nini Kansela Merkel anatoa picha ya maafa juu ya Umoja wa Euro, ikiwa Wasoshalisti watashinda katika uchaguzi nchini Ufaransa? Gazeti hilo linasema huo ni upuuzi.

Linaeleza kuwa ni jambo la kushangaza kwamba Kansela Merkel ameamua kuunga mkono upande mmoja, lakini ule upande unaotumia kila fursa kujijengea umaarufu kwa kuisifu kila njia inayotumiwa na Ujerumani.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Othman Miraji