1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Tutawalida Wayahudi na Waislamu wa Ujerumani

15 Januari 2015

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameahidi kuwalinda Wayahudi na Waislamu wanaoishi nchini Ujerumani dhidi ya ubaguzi.

https://p.dw.com/p/1ELEA
Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Amesema demokrasia ndiyo njia bora ya kupambana na machafuko yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali, kama yale matukio ya nchini Ufaransa wiki iliyopita.

Kauli hiyo ameitoa leo baada ya bunge la Ujerumani-Bundestag, kuwakumbuka kwa dakika moja wahanga 17 waliouawa katika mashambulizi ya wiki iliyopita mjini Paris. Merkel amesema Uyahudi na Uislamu vyote ni sehemu ya Ujerumani na ameahidi kwamba suala la kupambana na Uyahudi na mashambulizi dhidi ya misikiti litakuwa na mashtaka sawa.

Akizungumza wakati wa kikao hicho cha bunge kilichohudhuriwa na balozi wa Ufaransa nchini Ujerumani na viongozi wa kidini, Merkel amesema Ujerumani na Ufaransa zinahusiana kutokana na urafiki muhimu walionao.

''Ujerumani na Ufaransa zinasimama pamoja wakati wa matatizo haya magumu. Ujerumani na Ufaransa zinasimama pamoja zikijua wazi kwamba Ujerumani haiwezi kuwa na usalama, iwapo hakuna usalama Ufaransa, alisema Merkel .''

Kansela Merkel amesema ni muhimu pia kwa viongozi wa dini ya Kiislamu kuandaa mwongozo wa wazi unaotofautisha kati ya Uislamu na ugaidi. Amesema watu wengi nchini Ujerumani siyo maadui wa Uislamu, ingawa watu wanataka kujua ni kwa nini magaidi hawana huruma na maisha ya binaadamu. Amesema viongozi hao wanapaswa kueleza ni kwa nini mara nyingi ghasia zinafanyika kwa kutumia imani yao.

Merkel na wabunge wa Ujerumani wakiwakumbuka wahanga wa Paris
Merkel na wabunge wa Ujerumani wakiwakumbuka wahanga wa ParisPicha: Reuters/F. Bensch

Ujerumani haitoyumbishwa na vitendo vya itikadi kali

Amebainisha kuwa Ujerumani haitoyumbishwa kwa vitendo vya itikadi kali na itahakikisha inapambana na mahubiri ya chuki, vurugu na ghasia zinazofanywa kwa kutumia jina la Usialmu na wale walio nyuma ya ghasia hizo. Merkel amesema hatua zilizochukuliwa na Ujerumani na Ulaya ili kuweka ulinzi dhidi ya kitisho cha ugaidi na Uislamu wenye itikadi kali, hazitowaruhusu magaidi kuigawa jamii.

Amesema baada ya kufanikisha hatua ya kupiga marufuku watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Jihadi, baraza lake la mawaziri litaweka adhabu kali kwa watu wanaofadhili ugaidi. Hata hivyo, Ujerumani itaendelea kutoa msaada wa silaha na mafunzo ya kijeshi kwa majeshi ya Wakurdi wanaopigana na kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu-IS, nchini Iraq na Syria.

Aidha, Kansela Merkel ameunga mkono wazo la kuwepo uchunguzi zaidi wa data za mtandaoni ili kupambana na ugaidi na katika hatua za kuhakikisha usalama. Ametoa wito wa kuanzishwa upya hatua za kuwaruhusu maafisa kuficha data, suala ambalo wakosoaji wanasema huenda likahujumu uhuru wa vyombo vya habari na kukiuka haki za kimsingi za umma.

Mashambulizi ya Paris yametokea wakati ambapo Ujerumani ikitathmini namna ya kukabiliana na maandamano katika mji wa mashariki wa Dresden yanayoongozwa na kundi linalopinga Uislamu linalojiita PEGIDA.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman