1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani anakutana na vuongozi wa Uturuki

18 Oktoba 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumapili (18.10.2015) yuko kwenye mazungumzo na viongozi wa Uturuki kutafuta njia za kuutatuwa mzozo wa wahamiaji kufuatia kukatishwa tamaa kwa Uturuki na juhudi za Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1Gq7G
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu katika mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul. (18.10.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu katika mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul. (18.10.2015)Picha: Reuters/M. Sezer

Merkel ameanza kukutana na Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu katika Kasri la enzi ya utawala wa Ottoman la Dolmabahce mjini Instanbul kabla ya kuwa na mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan katika ziara yake hiyo muhimu ya siku moja ambayo ilitangazwa hapo tarehe 12 mwezi wa Oktoba.

Waziri Mkuu huyo wa Uturuki ameupongeza msimamo mzuri wa Umoja wa Ulaya katika kushirikiana mzigo wa mzozo wa wakimbizi kufuatia mazungumzo yake na Kansela Merkel.

Davutoglu amekaririwa akisema "Kwa bahati mbaya Uturuki ilikuwa imeachiwa peke yake na jumuiya ya kimataifa katika suala la kushirikiana mzigo huo. Tumeridhishwa sana kwamba sasa kuna mtizamo mzuri zaidi wa suala hilo. Suala la kushikiana mzigo huo ni muhimu sana."

Umoja wa Ulaya na Uturuki hivi sasa zinajaribu kukubaliana juu ya mpango kwa serikali ya Uturuki kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji ili badala yake nchi hiyo ipatiwe msaada mkubwa wa kifedha.

Matumaini ya maafikiano

Davutoglu amesema ana imani watapata matokeo mazuri ya malengo hayo.Amempongeza Merkel kwa kutolifumbia macho suala hilo la mzozo wa wakimbizi.Ameongeza kusema kwamba watu wengine wengi walisema wakimbizi hao wanapaswa kurudishwa makwao kutoka Umoja wa Ulaya na kwamba Merkel ameonyesha msimamo wa ubinaadamu.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Istanbul. (18.10.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Istanbul. (18.10.2015)Picha: Reuters/B. Kilic

Merkel kwa upande wake amesema Uturuki hadi sasa imekuwa na msaada mdogo wa kimataifa kwa mchango ilioutowa katika kuwahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni mbili kutoka Syria. Amesema haikuwa kwa maslahi ya pande zote mbili kwa mzozo huo kuja kuzalisha wahamiaji wasio halali wanaokimbilia Ulaya.

Ameendelea kusema " hili haliwezi kuwa ndio lengo.Titajihusisha kwa nguvu zaidia kifedha kama Umoja wa Ulaya.Ujerumani itatimiza wajibu wake."

Wakati kukiwa hakuna dalili ya kumalizika kwa mzozo huo ambao umetowa changamoto kubwa kabisa kwa uongozi wa Merkel mmiminiko wa wahamiaji na wakimbizi unaendelea kuingia barani Ulaya kwa kupitia Slovenia baada ya Hungary kuufunga mpaka wake na Croatia.

Usalama wa mipaka

Umoja wa Ulaya unaitaka Uturuki kuchukuwa hatua zaidi kuimarisha usalama wake wa mipaka na kuisaidia kudhibiti mmiminiko huo wa wahamiaji kutoka Syria,Iraq na nchi nyengine zenye mizozo wakitaka hifadhi katika Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Istanbul. (18.10.2015)
Wahamiaji na wakimbizi wakikimbilia kwenye mpaka wa Austria wakitokea Hungary.Picha: Reuters/L. Foeger

Kwa upande wake Uturuki inataka kutambuliwa zaidi kwa dhima yake ya kuwapokea zaidi ya wakimbizi milioni mbili kutoka Syria,kuongezewa msaada wa kifedha na kuharakisha mchakato uliokwama wa nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Ujerumani kimekuwa kituo kikuu chenye kukimbiliwa na wakimbizi wengi ambao wengi wao wanasafiri kupitia Uturuki na nchi za Balkan na inategemewa kusajili watafuta hifadhi zaidi ya milioni moja mwaka huu jambo ambalo limemuathiri kisiasa Angela Merkel.

Akionekana kutozipa uzito juhudi za Umoja wa Ulaya kakabiliana na mzozo huo wa wahamiaji Rasi Erdogan wa Uturuki ameutaka umoja huo kulipa uzito zaidi suala la Uturuki kuomba uwanachama kwa umoja huo. Alikaririwa akisema " Tumewapa hifadhi wakimbizi milioni 2.5 lakini hakuna mtu anayejali."

Masuala mengine katika agenda

Wakati Uturuki ikikabiliwa na awamu ngumu ya maisha yake katika historia yake ya kisasa Merkel pia anatarajiwa kujadili suala la usalama ikiwa ni wiki moja baada ya miripuko miwili ya mabomu kuuwa zadi ya watu 100 nchini humo wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwezi wa Novemba.

Wahamiaji wakihatarisha maisha yao kuvuka bahari ya Mediterenia kuingia Ugiriki.
Wahamiaji wakihatarisha maisha yao kuvuka bahari ya Mediterenia kuingia Ugiriki.Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Taasisi za utafiti zinasema iwapo Ujerumani na Uturuki zitashindwa kufikia makubaliano hakuna tena ufumbuzi unaonekana kwa mzozo huo na mmiminiko wa wahamiaji kutoka Syria na kwengineko kuingia Ulaya utaendelea.

Zaidi ya watu 630,000 wanaokimbia vita na shida Mashariki ya Kati na Afrika wamewasili kwenye fukwe za Ulaya mwaka huu wengi wakifunga safari kwa kuhatarisha maisha yao kwa kuvuka bahari ya Mediterenia.

Watu wengine 12 wamezama nje ya mwambao wa Uturuki hapo Jumamosi na hapo Jumapili walinzi wa mwambao wa Ugiriki wamesema wahamiaji watano akiwemo mtoto mchanga na wavulana wawili wamekufa wakati wakijaribu kuvuka bahari ya Aegean.

Wale wanaofanikiwa kuingia Ulaya wengi wao hujaribu kwenda Ujerumani baada ya Merkel kutangaza wazi kwamba nchi yake itawapokea watu wanaokimbia umwagaji damu nchini Syria.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP

Mhariri : Oumilkheir Hamidou,