1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Afrika Kaskazini

2 Machi 2017

Kansela wa Ujerumani anatembelea mataifa mawili ya Afrika Kaskazini kutafuta washirika katika mgogoro wa wakimbizi. Lakini kwa mara nyingine tena, wanaoweza kuwa washirika wake wamegubikwa na utata.

https://p.dw.com/p/2YVII
Merkel ziarani Misri
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Merkel anasafiri Alhamisi kuelelea nchini Misri, na siku ya Ijumaa ataizuru Tunisia, akiwa na malengo tofuati; miongoni mwayo ni kuzungumza na utawala nchini Misri kuhusu nchi jirani ya Libya inayokumbwa na vita, ambako watu wengi hukimbia mapigano kila siku na kuelekea  Ulaya kupitia bahari ya Mediterrania. Bila ya kuwepo na utulivu nchini Libya, ni vigumu kuwazuwia wafanyabiashara wanaochukuwa fedha nyingi kutoka kwa watu hao na kuwapadisha kwenye maboti yasio salama kuwalepeka Ulaya. Kwa sasa Misri inamuunga mkono Jenerali mwenye utata  Khalifa Haftar.

Kwa upande mwingine Merkel anahitaji yumkini kuzungumzia juu ya wakimbizi na hatimae kujadili makubaliano kama yaliyofikiwa na Uturuki. Uharaka wa Merkel unashadidiwa siyo pekee na kishindo cha uchaguzi mkuu wa Ujerumani hapo Septemba, bali pia chaguzi za nchini Ufaransa na Uholanzi, ambako wagombea wa siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia kama vile Marine Le Pen na Geert Wilders wanazidi kuungwa mkono kwa kuchochea hisia kali dhidi ya mpango wa wakimbizi wa Merkel, anasema  Joachim Paul, mkuu wa Wakfu wa Heinrich-Böll katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis. "Serikali ya Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya wanajribu kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kunakuwepo na mabadiliko katika sera ya uhamiaji. Katika hili Umoja wa Ulaya umeainisha mpango wake kuhusu Libya, na katika waraka maalumu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya zimebainishwa hatua za kuchukuliwa katika eneo la Afrika kaskazini ili kuzuwia wakimbizi na wahamiaji kuingia Italia na Ugiriki kupitia bahari ya Mediterrania."

Usalama Misri bado tatizo

Uchumi wa Misri unategemea utalii kwa kiwango kikubwa
Uchumi wa Misri unategemea utalii kwa kiwango kikubwaPicha: picture-alliance/dpa

Merkel aliisifu Misri kuwa nchi inayoleta utulivu katika kanda inayogubikwa na migogoro na hivyo ipo haja ya kushirkiana na rais Abdel-Fattah Al-Sissi. Lakini watetezi wa haki za binaadamu wanaukosoa mpango huo, ambapo shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch liliushutumu utawala wa Al-Sissi kwa kuhusika na ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binaadamu katika historia ya sasa. Paul anaelezea mashaka iwapo hata ikiwa vituo vya kuzuwilia wakimbizi vinaweza kuendeshwa nchini humo kwa kuzingatia vigezo vya chini kabisaa vya ulinzi wa haki za binadamu. Anasema hata usalama wa Misri chini ya utawala wa Al-Sissi umedorora zaidi badala ya kuboreka.

Anasema mapambano ya utawala huo dhidi ya ugaidi hayaelekezwi tu kwa makundi ya kigaidi, bali pia yanatumiwa kuhalalisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani wasiotakiwa, na kuongeza kuwa ipo haja ya kuangalia kwa umakini iwapo nchi ya Misri ambayo Ujerumani inataka kushirikiana nayo kweli inao utulivu na iwapo ni jambo la busara kuingia makubaliano na nchi kama hiyo na kuusaidia utawala wake.

Makubaliano kuhusu waomba hifadhi

Raia wa Tunisia wapinga waliohusishwa na ugaidi je ya nchi kurejea nchini
Raia wa Tunisia wapinga waliohusishwa na ugaidi je ya nchi kurejea nchini Picha: Getty Images/F.Belaid

Haijabainika wazi iwapo suala la kuanzisha vituo vya kuzuwilia wakimbizi litakuwa pia kwenye agenda ya Merkel nchini Tunisia au la. Wakati Merkel alipompokea waziri mkuu wa Tunisia Youssef Chahed mjini Berlin karibu wiki mbili zilizopita, suala hilo halikugusiwa katika mazungumzo yao, na katika mahojiano na shirika la habari la FAZ, Chahed binafsi alipinga mpango kama huo akisema si wazo zuri.

Kwa mtazamo wa Ujerumani, taifa hilo dogo kabisaa la Afrika Kaskazini lina umuhimu wa kipekee. Tunisia ni taifa pekee la Afrika Kaskazini lililofanikiwa kutekeleza demokrasia na mageuzi baada ya mapinduzi ya umma yaliyoyakumba mataifa kadhaa ya Kiarabu. Hivyo, anasema rais wa chama cha Ujerumani na Tunisia Raouf Khammasi, "Hatutarajii kwamba mazungumzo yatajikita tu katika sera ya uhamiaji. Kwanza ya yote anataka mazungmzo hayo yajikite katika kuboresha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, na kusaidia ujenzi wa miundombinu ya demokrasia."

Suala lingine ambalo Merkel anapaswa kulijadili nchini Tunisia ni kuhusu kurejeshwa kwa waomba hifadhi ambao maombi yao yalikataliwa nchini Ujerumani. Ingawa idadi yao ni ndogo, wakiwa karibu 1,500, suala hilo limezusha mjadala mkubwa nchini Ujerumani baada ya tukio la mashambulizi katika soko la Krismass mjini Berlin ambapo Mtunisia Amri Anis aliendesha lori na kuwagonga watu na kuuwa 11 na kujeruhi wengine zaidi ya 30.

Mwandishi: Stephanie Höppner

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf