1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani China

Halima Nyanza16 Julai 2010

Kansela wa Ujerumani ameitaka China kurahisisha upatikanaji wa masoko yake, wakati taifa hilo ambalo ni la pili dunia kwa usafirishaji wa bidhaa nje, likitia saini mfululizo wa makubaliano, yenye thamani kubwa.

https://p.dw.com/p/ON6d
Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao akiwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, baada ya kusimamia utiaji saini, makubaliano mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.Picha: AP

Baada ya kukutana kwa mazungumzo na Waziri mkuu wa China mapema leo na kusimamia utiwaji saini makubaliano kuhusiana na masuala ya biashara, nishati na masuala ya utamaduni, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitizia matumaini ya Ujerumani kwa China.

Amesema makampuni ya China kama yalivyo ya nchi nyingine duniani yanafurahia upatikanaji mzuri wa masoko ya Ujerumani, na kuongeza kwamba wana matumaini kuwa wajasiriamali wa Kijerumani nao pia wanaweza kupata nafasi kama hiyo katika masoko ya China.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na China biashara kati ya mataifa hayo imekuwa haraka hadi kufikia dola bilioni 91 mwaka uliopita kutoka dola bilioni 41 katika kipindi cha mwaka 2001.

Kwa upande wake Waziri mkuu wa China Wen Jiabao akizungumza katika mkutano wake na Kansela Merkel alisema wana matumaini kuwa biashara kati ya nchi hizo mbili itakuwa katika viwango vlivyo sawa na kufuata sheria.

Aidha akizungumzia kuhusu sarafu ya Euro, Wen Jiabao amesema nchi yake imekuwa na imani na sarafu ya Euro na kuongeza kwamba bara la Ulaya litaendelea kuwa moja ya masoko yao ya uwekezaji.

Lakini hata hivyo China imesema itaendelea kufuata msingi wake wa kuwa na akiba ya kuweka sarafu mbalimbali.

Akijibu kuhusiana na sarafu ya Euro, kansela wa Ujerumani amesema kiongozi huyo wa China kuwa na imani na sarafu hiyo ni dalili muhimu kwamba China ina imani na Euro na kuelezea pia juhudi za umoja wa Ulaya kuimarisha sarafu yake hiyo.   

Bibi Merkel amesema pia kwamba Ujerumani na China wameimarisha uhusiano wao katika misingi mipya na kwamba ushirikiano wao unapangwa kuimarishwa zaidi katika mashauriano ya kila mwaka baina ya serikali za nchi hizo mbili.

Na katika taarifa yao ya pamoja, nchi hizo mbili zimeahidi ushirikiano wa karibu katika siasa, hususan katika kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa.

Ziara hiyo ya bibi Merkel nchini China, inafanyika, baada ya mwaka 2007, China kuvuruga uamuzi wa Kansela Merkel kukutana na kiongozi wa kiroho wa Tibeti, Dalai Lama, ambapo China wanamchukulia kama muasi hatari.

Hata hivyo hali hiyo ya mvutano wa China na Ujerumani imeonekana kuondoka, baada ya Ujerumani kuthibitisha kuunga mkono sera ya China na maadili katika nchi ya China.                                                   

Mwandishi: Halima Nyanza(afp,adp)

Mhariri:Josephat Charo